Wakati
tunapoaminishwa kwamba dunia kwa sasa inakwenda kasi kuliko wakati wowote na
yawezekana ni kweli, na wakati tunapoambiwa na wataalamu wa tabia za binadamu
kwamba uwezo wa akili na ubunifu wa mtu unapungua kwa kadri umri wake
unavyoongezeka na hivyo kwamba mafanikio yana umri, hali halisi ni tofauti
kabisa.
Ukisoma
Biblia utaona kwamba Musa aliyewakomboa Israel hakuanza kazi hiyo hadi
alipokuwa na umri wa miaka themanini. Alitumia miaka arobaini ya kwanza ya
maisha yake nyumbani mwa Farao akifundishwa jinsi ya kuwa na kuishi kama
mtawala. Historia inaonyesha kwamba katika kizazi cha musa (Mnamo 1520BC) Misri
ndilo taifa lililokuwa limestaarabika na likiitawala dunia, hawa ndiyo walikuwa
mabingwa wa elimu, uchumi na utawala na Musa alizaliwa na kulelewa ndani ya
ikulu ya utawala wa dunia wa wakati huo. Hii ni kusema Moses alikulia ikulu
akifundishwa kufanya biashara, kupigana vita, kuamua mashauri na mafunzo
mengine waliyofunzwa watoto wa ikulu ya farao Amunhotep I aliyeitawala Misri
kati ya mwaka 1532-1511BC na Farao Tuthmosis II aliyetatufa kumuua Musa mnamo
1486 na hivyo Musa kulazimika kukimbia Misri.
Wakati
naisoma historia ya Musa, nikajifunza mambo kadhaa ambayo naona kama yana maana
sana kwa kijana anayehangaika na suala la kujitambua na kuutambua wito wake
katika maisha.
Navutwa
kuamini kwamba siyo kweli kwamba Musa hakuifahamu historia yake hasa kwa
kuzingatia kwamba alilelewa miaka yake ya awali ya utoto wake kwenye nyumba ya
baba na mama yake ambao walikuwa Waebrania. Najua, nimesema hapo mwanzo kwamba
Musa alikulia kwenye ikulu ya farao, lakini biblia iko wazi juu ya maisha ya
utoto na msingi wa malezi ya Musa ulikuwa wapi. Kut: 2: 5-9.
“ Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake
wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma
kijakazi wake kwenda kukileta. Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi
akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. Basi umbu lake mtoto akamwambia binti
Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako,
akunyonyeshee mtoto huyu? Binti
Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule
mtoto. Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee,
nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe.
Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini”.
Biblia inatwambia yule mtoto “akakua” lakini haisemi
alikua kiasi gani na ni sahihi kufikiri kwamba wanawake wa kizazi kile
walinyonyesha watoto muda mrefu kuliko leo, basi yawezekana kwamba Musa aliishi
nyumbani kwa baba na mama yake muda mrefu sana. Lakini pia kwa sababu Musa na
Haruni na Miriam wanaonekana kuwa na mahusiano imara hata wakati Musa aliporudi
kutoka Midian, ingekuwa sawa kudhani kwamba upendo wao na makuzi yao wakati wa
utoto ndivyo vitu vilivyojenga mahusiano haya wakiwa wakubwa.
Lakini Biblia inatuonyesha kwamba “Hata siku zile, Musa
alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao……”
Kutoka: 5:11. Mwandishi wa waraka kwa Waebrani analiweka sawa zaidi hil
anaposema “….Musa alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti farao….”.
Ebr 11
Biblia inasema Musa alipokuwa mtu mzima, aliamua kufanya
maamuzi kadha wa kadha ambayo yalimpeleka kwenye wito wake katika maisha.
Nilijifunza kupitia mstari huu kwamba Musa hakuanza kujitambua hadi alipofika
umri wa miaka arobaini. Ni katika umri huu ambapo Musa anatoka na kwenda
kuwatazama ndugu zake na labda hilo halikutarajiwa kwa mwana wa mfalme, labda
pia kwa vile alikuwa ameasiwa kwenye familia ya kifalme na kila mmoja kwenye
familia akijua kwamba hakuwa Mmisri, kwake yeye kuwatembelea Waebrania
kulifanya wanausalama wa Misri kuchunguza mienendo yake zaidi?. Lakini Musa
akijua kwamba yeye kuwatembelea waebrani inahatarisha maisha yake na nafasi
yake, bado alitoka akaenda kuwatazama na alichokiona kikawasha moto uliokuwamo
ndani yake muda mrefu. Moto wa kutotaka kuona Waebrania wakionewa, moto wa
kutamani nao wawe watu huru, moto wa kutamani waishi na kuheshimiwa utu wao,
ukawasha na ugomvi mdogo tu kati ya Mmisri na Muebrania.
Ni jambo gani ambalo linakukera na unadhani ukipata
nafasi utalibadili kabisa katika familia yako, katika jamii yako, katika taifa
lako!?. Ni kitu gani ambacho ukikifanya katika jamii yako na kukikamilisha
utajisikia umeishi maisha kwa ukamilifu? Kwa wengine ni kuwa daktari bingwa na
kuweza kuwatibu watu aina fulani ya ugonjwa, kwa mwingine ni kuweza kujenga
kiwanda cha kusindika mazao ya watu wake wanaoteseka na kulima bila kuwa na
soko la mazao hayo, kwa mwingine ni kuwa hakimu ama mwanasheria kuwapa haki
wanaoonewa na kwa mwingine ni kuwa kiongozi bora wa familia yake na kuwa mume
bora na baba bora wa watoto wake na kadhalika. Kuna majira na wakati kwa jambo
hilo na unaweza kuanza sasa. Yawezekana ukakosea mara kadhaa, yawezekana
ukashindwa mara kadhaa na yawezekana katika kuanza ukajikuta umeharibu kabisa,
lakini usiibadili talanta yako na ya mwingine, ama usiyapunguze maono yako
kiasi cha kutafuta chakula na mavazi tu, una kitu cha ziada cha kufanya kuliko
hayo.
Kama unasoma makala haya, maana yake ni kwamba mimi
walau nimefanikiwa kuandika na kuchapisha makala yenyewe, lakini huwezi kuamini ni
vingapi havikufika hata kwa mchapishaji, ni vingapi hata sikuandika zaidi ya
kurasa mbili, ni vingapi vilipotelea kwenye mikono ya watu nilioamini
wangenisaidia kuvichapa na wao wakavitupa kwenye majalala kwa kuviona takataka.
Huwezi kujua ni makala ngapi niliandika na zilipotoka
magazetini nikajiongezea maadui, huwezi kujua ni maandiko mangapi yalinifanya
kupoteza marafiki, kufukuzwa kazi, kunyimwa nafasi kwenye maisha na kadhalika,
lakini sikuacha kuandika. Sikuacha kuongea na watu hata kama walikuwa wawili
tu, sikuacha kuanzisha mijadala iwe kwenye vyombo vya usafiri, kwenye nyumba za
ibada, kwenye ofisi na mahala pa kazi, na hata mara nyingine nikihubiri na
kuhutubia viti na meza sebleni kwangu kwa sababu nilikuwa na kitu cha kusema na
haja ya kusikizwa.
Mpaka hapa nadhani tumeelewana kwamba kuna kusudi ndani
ya kila mtu, kuna talanta ama kipawa
kilicho ndani yako. Nataka kurudi nyuma kidogo nikwambie mambo mawili kuhusu talanta
na kisha twende kwenye swali linalofuata.
Turudi kidogo kwenye habari za Musa aliyewatoa Israel
kutoka utumwa wa Misri. Nimesema hapo mwanzo kwamba naamini alijifahamu kwamba
kukulia kwake ndani ya ikulu ya Misri ilikuwa “bahati” tu hasa kwa vile alikuwa
Mwebrania. Lakini yawezekana kwamba hakuwa na mkakati wowote wa kuwakomboa watu
wale kutoka utumwa na hivyo pamoja na kuwahurumia, lakini hakuwa na kusudi la
kuwaokoa wala hakuwa na mpango wowote.
Unasema najuaje haya!? Kwanza kwa sababu ni pale tu
“alipokuwa mtu mzima” (alipojitambua, alipojihoji na kuona lile shimo tupu ndani ya moyo kwamba ajapokuwa anaishi kwa
anasa kwenye jumba la kifalme lakini bado hakuwa na ridhiko halisi la moyo)
ndipo alipoamua kujitanabahisha na watu wake hasa ambapo mwandishi wa waraka wa
Waebrania anasema “…aliona ni sawa kuteseka na watu wa Mungu…..” Hii
inamaanisha kwamba pamoja na kwamba alikuwa na nafasi, ujuzi na hata uwezo
lakini alikuwa hajawa na utayari wa kuteseka na watu wake na hivyo aliona bora
kula na kulala vizuri huku akiumia moyoni juu ya watu wake.
Nimejifunza katika maisha yangu binafsi kwamba pana
nyakati ambazo unaweza kuwa unafurahia kwa nje mazingira fulani ya raha uliyo
nayo, lakini mazingira hayo hayakupi furaha wala riziko la moyo.
Kuna wasichana wengi ambao wako kwenye mahusiano na
wanaume watu wazima kuliko wao na labda waume za watu kwa sababu ya furaha ya
kupewa fedha na kutimiziwa mahitaji yao kadhaa, lakini hawana ridhiko la moyo.
Wana raha lakini hawana furaha. Ni ajabu pia kwamba wengi wa hawa, wana ujuzi
na vipawa kadha wa kadha ambavyo vingewapa nafasi katika jamii yao na hata
kuwafungulia milango ya kupata mahitaji yao, bila kulazimika kuwa watumwa. Kuna vijana wengi walio kwenye matumizi ya
madawa ya kulevya na kadhali kwa sababu wamekatishwa tamaa na muda wakidhani
wamepitwa na wakati wao wamepitwa na muda wa kutumia vipawa vyao na katika ati
kutafuta kujifariji, wamekuwa watumwa wa madawa ya kulevya na uharibifu
wake.
Nimesikia na kusoma juu ya wanawake wengi waliokuwa kwenye
ndoa za mitala bila kutaka kwa vile tu walikuwa na mahitaji ama ya kiuchumi,
ama ya kijamii kwa maana ya heshima na ulinzi wa kuwa na mume, mara wanawake
hawa walipogundua nguvu ya maamuzi katika kumwamini na kumwishia Mungu, na
maisha yao yamebadilika.
Nilikutana na dada mmoja mkoani Tabora nchini Tanzania,
yeye alikuwa binti mkristo ambaye aliamua kuolewa ndoa ya mitala kwa sababu ya
hali ngumu ya uchumi na ugumu wa maisha. Alikaa kwenye ndoa hiyo kwa miaka
zaidi ya saba hadi aliporudi kwa Kristo tena, hapo akaamua kwamba alikuwa na
ndoto ya kuwa nesi maisha yake yote na kuamua kwenda kusomea unesi, leo
mwanamke huyo ni nesi kwenye hospitali kuu ya mkoa, ameolewa na mwanaume wa
ndoto zake na wana familia nzuri inayojiweza. Kifungo cha uchumi kimevunjwa na
kutambua ndoto, kipawa na wito wa mwanamke huyu, wakati wa kuutekeleza na
maamuzi ya kuanza na kufanya.
Jambo la pili ni kuzielewa hatua za kujitambua.
Kujitambua kwa mtu naweza kukufananisha na mfumo wa namna ambavyo kipepeo
hubadilika kutoka Rava hadi kuwa mdudu mwenye mabawa na kupaa. Ni mchakato. Pia
kujitambua hakuna mwisho kwa sababu ni ugunduzi wa uwezo uliomo ndani yako kwa
nyakati tofauti za maisha. Unaweza kufanya kila kitu katika maisha, isipokuwa
kwa aina na viwango tofauti kulingana na hatua uliyopo katika maisha.
Musa hakuwa
akiishi ikulu akijiandaa kutoka na kuwakomboa watu wake, aliishi na kutumikia
utawala wa Misri na labda akitumaini siku moja kuwa mtawala wa Misri, hadi siku
moja alipojaribu kuwasuruhisha waebrania waliokuwa wakigombana na kuishia
kufukuzwa ndani ya Misri akiwa na mavazi yake tu. Labda aliwaza kuchukua kiti
cha Misri siku moja na kisha kuwaachia Waebrania waende zao huku yeye akibakia
Misri. Labda alijitia moyo kwa historia ya Yusufu ambaye japo hakuwa Mmisri, hakuwa
amelelewa ikulu ya Misri, hakuwa na mafunzo ya utawala ya Kimisri, lakini
alitawala Misri na katika utawala wake ndugu zake waliishi vizuri, lakini Mungu
alikuwa na lengo tofauti kabisa.
Kutoka 2: 11-15 “Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu
mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri
anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi
akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule,
akamficha ndani ya mchanga. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania
walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga
mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na
mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa
akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. Basi Farao alipopata habari, akataka
kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya
Midiani; akaketi karibu na kisima”
Inaendelea.......!!!!
No comments:
Post a Comment