Karibu. Tunaendelea na mfululizo wa somo letu juu ya Jinsi gani kijana aisafishe njia yake!? Kama utakavyoona huko mbeleni, kama hakuna "uchafu" kwenye njia, bila shaka Daudi asingetushauri kuzisafisha njia zetu. Na pia tusingehitaji kuzitambua na kuzisafisha njia kama hakuna tunakokwenda. Karibu, uendelee kujisomea.
Kwanini niliumbwa?
Swali la
pili katika juhudi za kujitambua ni kwanini uliumbwa na kwanini umeumbwa
ulivyoumbwa?.
Kuna misemo
mingi na maelezo mengi sana kuhusu kwanini. Kwanini huwa mwanzo wa udadisi ama hasi au chanya kwa yule
anayeuliza. Kwanini imekuwa chanzo cha vumbuzi nyingi tuzionazo duniani leo.
Mtafiti na mwanasayansi aliyegundua mawasiliano ya simu, alisukumwa na kwanini
asiweze kufikisha mazungumzo ya sauti umbali umbali mrefu zaidi na leo tunazo
simu za viganjani, madaktari bingwa wa madawa ya utabibu na kemia husukumwa na
kwanini katika kuanza tafiti zao ambazo huwa msaada mkubwa kwa matatizo ya
binadamu na kadhalika.
Hata kijana
katika juhudi za kujitambua, yapaswa kujiuliza swali hili mara nyingi kwa kadri
uwezavyo. Swali hili ndilo hufanya watu kusafiri mwendo mrefu, kufika mbali
katika taaluma na kadhalika kwa kujihoji ni kwanini niliumbwa.
Je!
Niliumbwa ili nile, nilale, nijenge nyumba na kuishi ndani yake, niliumbwa
niishi, nizeeke, nife, ama niliumbwa nifanye jambo fulani katika maisha
yangu!?.
Ili kujibu
swali la kwanini uliumbwa, unahitaji kwanza kutambua mambo kadha wa kadha
yanayokutofautisha na watu wengine. Katika maisha kila mtu anao uzoefu wake,
uzoefu wako mpaka hapo ulipofika unaweza kukwambia mengi kuhusu wewe. Nakumbuka
wakati nilipokuwa mdogo, nilipokuwa mdogo, nilipenda kukaa na kusikiliza
mijadala ya watu wazima, na kwa vile nililelewa na bibi yangu ambaye hakusita
kujibu swali lolote nililomuuliza, si ajabu nikiwa na umri wa miaka tisa tu
nilihubiri somo langu la kwanza kwenye mkesha wa usiku mbele ya waumini
wasiozidi ishirini. Kwangu hilo lilikuwa fanikio kubwa, miaka ishirini baadaye,
nimeweza kuzungumza na umati wa watu kwenye maeneo mengi, nimekuwa kwenye
mikutano kadha wa kadha yenye changamoto na watu wamesema vyema juu ya
uzungumzaji wangu na sasa nimejifunza kwamba kumbe mimi ni msemaji.
Ni pale
nilipogundua kwamba watu wanalipwa mishahara mikubwa kuwa wasemaji wa taasisi
kubwa duniani, nilipojifunza kwamba wahubiri wakubwa wanaishi maisha yao yote
kwa kuzungumza na wanasiasa hufanikiwa katika siasa pamoja na mambo mengine,
kwa kuwa wazungumzaji wazuri.
Ni baada ya
utambuzi huo nilipoanza kujifunza namna ya kuboresha uwezo wangu wa kuzungumza,
sijafanikiwa sana bado, lakini naweza kuzungumza na watu wengi, naweza
kuwafanya watu wanisikilize kwa muda mrefu, naweza kujua wakati wasikilizaji
wangu wanaponisikiliza kwa uvumilivu tu ama kwa kunielewa na shauku ya kuendelea
kusikia. Ningali najifunza, lakini walau nimetambua jambo.
Vivyo kwenye
maeneo mengine, katika kujiuliza wewe ni nani unahitaji kufahamu baadhi ya
mambo yanayokutofautisha na wengine na kukuhusianisha na wengine.
Leo
ninaandika makala na vitabu, lakini uandishi huu ni matokeo ya kupenda
kujisomea vitu vingi. Sisubiri taarifa yoyote inifuate, naitafuta ikiwa
ninaihitaji ama ninaitaka. Wakati nilipogundua kwamba nina tatizo la kujiamini
mbele ya watu na kwamba hilo lilikuwa likininyima uwezo wa kuwa bora kwenye
nafasi yangu, sikuwa na muda wa kwenda chuo kusomea lugha za alama lakini
nilikuwa na uwezo wa kupakua kutoka mtandao vitabu vya wataalamu kadha wa kadha
kuhusu somo husika, japo sijafaulu sana kwa jambo hili, lakini nimesaidika kwa
sehemu kubwa.
Najaribu kusema
kwamba kama ambavyo mashine zote duniani zimetengenezwa zilivyotengenezwa kwa
lengo moja tu la kuziwezesha kutekeleza lengo la kuundwa kwake, vivyo na wewe
umeumbwa ulivyoumbwa kwa ajiri ya kutimiza kusudi fulani katika maisha. Na kama tulivyoona hapo awali, ni rahisi
kulijua lengo ama kazi ya mashine fulani kwa kuuliza ama kusoma maelekezo
(Manual) ya mtengenezaji, na wewe muulize na soma neno la Mungu kwa ajiri ya
kujua lengo la kuumbwa kwako hivyo ulivyoumbwa.
Naona kama
tatizo kubwa la vijana ni kutozilisha akili zao aina sahihi za vyakula. Kama
hujui, chakula cha akili ni taarifa na unaweza kuilisha akili yako kwa vitu
vingi sana ikiwamo televisheni, magazeti, vitabu na mitandao. Mara nyingi
muonekano wa mwili wako husema sana ikiwa una afya ya kutosha ama lah! Na akili
yako pia inao uwezo wa kusema ikiwa inayo afya ya kutosha ama lah!.
Unahitaji
kula chakula bora, kupumzisha mwili wako, kuutunza kwa mavazi na kuuosha na
kadhalika na haya twayafanya mara nyingi, lakini ni ajabu kwamba linapokuja
suala la kuzilisha na kuzitunza akili zetu tunazembea. Vijana wengi hasa kwa
vile miaka yao ya mwanzoni ya ujana huwakuta mashuleni na vyuoni, hudhani
kwamba masomo ya shuleni yanatosha kuwafanya wao kuwa watu bora. Ndiyo, mitaala
ya masomo imeandaliwa kukufanya kuwa mtaalamu wa jambo fulani, lakini bado
unahitaji kujsomea vitu vingine kwa sababu utu wako unahusisha zaidi ya ufahamu
wa kawaida ama intellect, unahitaji pia imani na “….imani huja kwa kusikia, na
kusikia huja kwa neno la Kristo”
(Warumi 10:10), unahitaji hisia na kadhalika ili kuweza kushindana katika
ulimwengu wenye mashindano mengi kama huu.
Changamoto
nyingine ni pale ambapo kijana amesomea kitu ambacho siyo kile alichonacho
ndani ya utu na tabia yake. Wengi wa vijana hawana furaha japo wengine ni
wasomi, wenye ajira nzuri na zenye kuwawezesha kulipia gharama muhimu za maisha
yao na ziada. Ni changamoto kubwa Unapokuwa mtu anayependa kufundisha kama
mimi, mtu anayependa kushirikiana na wengine kile anachokijua, mtu anayependa kuchunguza
mambo ya kijamii na kujiuliza ama kutafiti ni kwanini jambo fulani katika jamii
fulani liko vile na siyo hivi na kadhalika, lakini mtu huyu anashinda
barabarani akijenga madaraja, ama akikadiria majengo ama akitengeneza mitambo
na mashine. Mara zote pamoja na kwamba atafanikiwa kukamilisha kazi yake,
atafanikiwa kumaliza ama kutimiza lengo la kazi husika, lakini hatopata ridhiko
la moyo kwa vile hakutumia nguvu zake kutenda kile ambacho hasa humpa ridhiko
kukifanya.
Nilimuuliza
Mhandisi mmoja juu ya aina fulani ya gari ambalo kwangu lilionekana kuwa na
tabia ya ajabu kwa utumiaji wake wa mafuta. Ikiwa gari hilo litatumika kwa
safari ndefu na kukimbia kwa mwendokasi mkubwa zaidi kidogo ya kawaida,
matumizi yake ya mafuta huwa chini, kuliko likitumiwa katika barabara za mjini
ambako mwendo wastani tu unatakiwa. Aliniambia gari hilo lilitengenezwa kwa
ajiri ya mwendo kasi na siyo mwendo mdogo ama wa wastani na hivyo kwa sababu ya
ukubwa wa injini yake, likiendeshwa kwa mwendo mdogo, halipati kufungua maeneo
yote yanayopaswa na hivyo kulazimika kutumia nguvu nyingi kusukuma na hivyo
kutumia mafuta mengi.
Mara
nyingine umehisi kama maisha yako yako polepole na kwamba hayaendi kwa kasi ya
kutosha!? Mara nyingine umehisi kama kile unachofanya katika maisha hakikupi
ridhiko la moyo na hivyo, mara nyingi umehisi kama lile gari kwamba unatumia
nguvu nyingi kuyasukuma maisha yako katika mwendo huu wa kuamka asubuhi, kwenda
kazini kwako, kufanya kazi unazopangiwa ama zilizopangwa, kurudi nyumbani na
kutazama televisheni na mara nyingine kuungana na rafiki zako kwenye mazungumzo
na kadhalika, na unapoamka kesho yake maisha yako kama yalivyokuwa jana
isipokuwa mabadiliko ya tarehe!?. Ndiyo, na huo ndiyo ukweli. Umeyaweka maisha
yako kwenye mduara na ni vugumu kuona mambo ama maeneo mapya kama unazunguka
kwenye duara. Ni pale tu unapofuata njia iliyonyooka kuelekea kule ambako
unapaswa kwenda, ndipo unapopata nafasi ya kuona vitu vipya, kukutana na
changamoto mpya njiani, kujifunza mambo mapya na kadhalika.
Ni kweli
kwamba ni muhimu kwako kama kijana kuwa na ama kujenga nyumba, kuwa na familia
na kusaidia ndugu na jamii yako, lakini safari yote ya maisha haiwezi kuwa tu
inalenga huko! Wako wengi wetu ambao uhisi kama maisha yana maana zaidi ya kula
na kulala, zaidi ya kuwa na kazi nzuri na mashahara mzuri na nyumba nzuri na
mke ama mume mzuri na kadhalika. Ni kwa hawa mfalme Daudi aliandika na
kuwashirikisha mawazo na maswali ya moyo wake aliposema “Ni jinsi gani kijana
aisafishe njia yake………!?” hasa kwa sababu alitambua kwamba maisha ni zaidi ya
kula na kulala bali ni safari. Siyo tu safari ya kuelekea mbinguni kama ambavyo
tumeamini kwa miaka dahali, bali ni safari ya kuuishia ufalme wa Mungu. Ufalme
ambao Mfalme wa ufalme huo Yesu Kristo hakuomba tuuendee, bali alitufundisha
tuombe kwamba ufalme huo uje duniani.
Sisemi
tusijitunze kwa usafi wa moyo kwa ajiri ya maisha baada ya kifo, bali nasema
kwa miaka tuliyomo duniani, yatupaswa kuuona utendaji wa ufalme wa Mungu kwenye
maisha yetu ya kila siku na ufalme huo kama alivyosema Kristo, unakaa ndani
yetu. Umemgundua mfalme aliyeko ndani yako!?.
Wengi
tunakumbuka jinsi ambavyo tulikuwa tukiambiwa tulipokuwa wadogo kwamba
tulitakiwa kusubiri hadi tuwe wakubwa ndipo turuhusiwe kufanya mambo fulani.
Bila shaka kulikuwa na hekima katika utaratibu huo, lakini kwa kadri siku
zinavyokwenda, maisha na mifumo yake imerahisisha kufanya chochote unachoweza
ama unachojisikia kufanya, almuradi huvunji sheria za nchi ama jamii yako.
Hata hivyo,
ukweli unabaki kwamba pana mambo ambayo hayahitaji tu uwezo ama ujuzi wa
kuyafanya, bali kama asemavyo Mhubiri; “Pana wakati na majira kwa kila kusudi
chini ya mbingu…..”
Inaendelea.........!
Kwa maoni na ushauri, tume ujumbe wako kwenye Whatsup No. 0788653649 au email: kamengegm@yahoo.com
No comments:
Post a Comment