Saturday, August 15, 2015

Jinsi Gani kijana kijana. 1 (4)



Ni kama mara nyingine Mungu hutumia mambo mabaya yanayotutokea kwenye maisha ili kutonyesha wito wetu hasa na kutuongoza kule ambako alitukusudia tangu kuwekwa misingi ya nchi. Tukiungana na Muhubiri kusema “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”,(Mhubiri 3:1) tunapaswa kujifunza pia kwamba kuna changamoto zitokanazo na mabadiliko ya wakati na majira kwenye maisha yetu.
Moja ya changamoto ambazo zimenikabili mimi binafsi katika maisha yangu, ni kuvitambua na kuishi kwenye vipindi vya mpito. Kwa sababu mimi ni mtu ambaye nimeishi aina nyingi za maisha, nimejifunza kwamba mara nyingi wakati tunapokuwa hatuna jinsi yoyote isipokuwa kutumaini katika Mungu, huo ni wakati mgumu sana kwetu. Lakini huo ni wakati mzuri pia kwetu kwa sababu hutusaidia kuonyesha uwezo wa utu wetu. Mara nyingi nimejua moyoni mwangu kwamba hali ya mazingira ama mahusiano inaanza kubadilika hapa nilipo na kwamba ni wakati wa kwenda hatua nyingine, lakini hofu yangu ya kuacha kile nilichokizoea, kubadili lile ambalo ni kawaida na kuchukua hatua kwenye sintofahamu, kwangu hiyo huwa changamoto kubwa. Binafsi nimekuwa nikilazimishwa na Mungu kubadilika na usidhani imekuwa rahisi hasa wakati wa mchakato husika. Haikuwa rahisi kwa Musa. Kwanza alikuwa mtu aliyeishi kati ya mawazo mawili kwa muda mrefu sana, na alikuwa na utambulisho usioeleweka. Usingemtanabahisha kama Mmisri kwa sababu hakuwa Mmisri kwa kuzaliwa na bila shaka katika maisha yake ya kila siku alikuwa akiambiwa kwamba kama siyo tu kufadhiliwa na binti Farao, basi angekuwa huko Gosheni akifyatua matofali na Waebrania wenzie.
Ni ajabu lakini ukweli mchungu kwamba watu watakupokea kwenye kariba yao kama hawana budi isipokuwa wanalazimishwa kukupokea, lakini hawatakuacha kusahau wewe ni nani. Watatumia kila nafasi waipatayo kukumbusha kwamba hukustahili kuwa hapo, watatumia kila mapungufu yako kukusimanga na kukufanya ujisikie mnyonge, japo kwa wasiojua watakuona kuwa mtu mwenye furaha sana lakini siri ya moyo wako unaijua mwenyewe.
Nakumbuka jinsi nilivyoishi kwa shida kwenye nyumba ya mmoja wa ndugu zetu aliyekuwa mtu mkubwa na kiongozi wa serikali wakati huo. Nilikuwa nimetoka kijijini kwa ajiri ya kusoma eneo la mjini ambako mama yangu alikuwa akifanya kazi, lakini kwa sababu ya udogo wa nyumba aliyokuwa akiishi mama yangu, mimi nililazimika kwenda kuishi kwa huyo ndugu. Nilikuwa darasa la tatu na pale nyumbani kulikuwa na watoto wa darasa langu na wengine wakubwa kidogo. Wakati wa kula, mimi nilipaswa kusubiri kwanza wao wamalize kula ndipo na mimi nile. Sikuweza kula baadhi ya vyakula ambavyo vilihesabiwa kuwa vya anasa kama maziwa, juisi, nyama na kadhalika isipokuwa mara chache tu ikiwa mwenye nyumba alikuwampo, ambapo nilipata pia nafasi ya kukaa na familia nzima sebuleni kwa ajiri ya chakula na kutazama televisheni.
Kama mwenye nyumba hakuwapo, na kwa sababu ya kazi na nafasi yake alikuwa akisafiri sana, niliishi kila sekunde kama mtumwa, kila mara nikikumbushwa kwamba nilikuwa mshamba niliyetoka kijijini na nisiyestahili kutangamana na wao. Mambo hayo pamoja na kwamba yaliniumiza moyo, lakini yamenifanya kuwa makini na watu ambao Mungu ananipa nafasi ya kuwasaidia kwa lolote, nimemwomba Mungu anipe neema nisiseme lolote la kuwatweza maana nayajua maumivu yake. Nimejifunza kwamba watu hatuwezi kufanana kufikiri na kutenda kwetu na hivyo ikiwa tunaishi pamoja, basi kumbe itatupasa kuvumiliana sana.
Naona kama Musa naye alikuwa na wakati wa namna hii. Wanahistoria wa utawala wa Misri wa wakati huo wanasema baada ya kifo cha Farao, mmoja wa wana wa mfalme angeweza kuchukua nafasi ya kuwa Farao wa Misri. Hili nalo bila shaka liliongeza shida kwa Musa hasa kwa vile baadhi ya wanahistoria wanasema Musa alikuwa na uwezo maalumu katika mapigano na busara ya utawala kuliko wenzake na hivyo alipopata tuhuma ya kuua mtu, tena kutoka kwa watu wake mwenyewe, sasa alikuwa na wakati mgumu zaidi, adui zake walikuwa wamepata sababu ya kumshambulia zaidi. Lakini pia yasemekana Farao Tuthmosis II alimpenda Musa na sasa alikuwa njia panda. Si ajabu ambavyo hata waliokuwa rafiki zako kwenye mamlaka hugeuka kuwa adui zako wakati wa kujiliwa kwako ukifika!?. Si ajabu kwamba sifa ileile iliyokufanya kuajiriwa, ndiyo sifa hiyo hiyo inayokufanya leo wanatafuta kukuaa!?. Kwani si ujuzi wa mapigano na uwezo wa maamuzi wa Musa uliokuwa umempa sifa mbele ya Farao, lakini haki ilipodai kwamba Mmisri ashughulikiwe kwa uwezo ule ule, moto ukawaka na Musa akajikuta hana kwao?.
Tambua Changamoto za wakati wako au kwa kusema sahihi, tafuta wakati wako ndani ya changamoto zako maana Mungu hataruhusu jambo litokee kwako ambalo hujaweza kukabiliana nalo. Huu ulikuwa wakati wa Musa kusogea hatua nyingine na hii haikuwa hatua nzuri sana kwa Musa lakini ilikuwa sahihi, ya lazima kwa ajiri ya kusudi la Mungu. Kutoka Ikulu hadi katika Jangwa la Moabu, mwana wa mfalme aliyegeuka mchunga mbuzi. Bila shaka Wamisri wangecheka sana kwa kusikia habari hizi. Lakini ni kipawa chake hiki hiki cha maamuzi, moyo wa kupenda kuona haki, moyo wa kutoona wanyonge wakionewa, ndivyo vilivyomfikisha kwa Yethro. Ni vipawa vyake hivi hivi vilivyoendelea kumtengenezea njia hata kwenye hatua hii. Mapenzi yake ya kuona haki inatendeka.
Kut 3: 16-22 “Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao.  Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao.  Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo?  Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula.  Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora.  Huyo akamzalia mwana, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni”. 

Tukutane kwenye sehemu tatu za mwisho katika sura hii ya kwanza kuanzia juma lijalo. 

No comments:

Post a Comment