Bwana Yesu Asifiwe, najua ni muda sijapost somo lolote hapa ndani, ni kwa sababu si kila mara napost isipokuwa tu Mungu anaponipa kitu cha kusema. Ebu shiriki na mimi somo hili jipya ambapo naamini litakujenga. Labda wewe ni kijana, mafunzo haya ni muhimu kwako, labda ni mzazi ama mlezi, itakusaidia kumtazama kijana unayemlea kwa jicho tofauti. Karibu.
Usijaribu
kumpendeza kila mtu, kimsingi usijaribu kumpendeza mtu bali Mungu. Moja ya
mambo ambayo yanawasumbua vijana wengi ni hali ya kutamani kukubalika na mtu
ama watu katika jamii yao hata kama wanalazimika kujikosea katika kutimiza
hilo.
Mara nyingine
jamii zetu, watu wanaotuzunguka na mara nyingine waliopaswa kutuongoza,
wanatushawishi kuacha kile tunachojua kwamba ni sahihi, ili tufanye kile
wanachodhani wao ndicho sahihi. Daudi alikumbana na hali hii. Wakati
alipokwenda kuwatazama ndugu zake vitani, kaka zake hawakupenda yeye kwenda
mstari wa mbele, hawakupenda yeye kuona wakishindwa vita, hawakupenda yeye
kuona wakitusiwa na kudhalilishwa na Mfilisti, na hivyo wakalazimisha Daudi
asisogee kwenye uwanja wa vita.
Hawakujua
kwamba Daudi pamoja na kwamba hakuwahi kupitia mafunzo ya kijeshi, alikuwa na
mbinu za mapambano kwa kupambana na Simba na Dubu waliovamia mifugo yake
machungani. Alikuwa na uwezo wa kuchukua kile alichojifunza kwenye maisha yake
kwenye hatua fulani, na kukitumia kwenye hatua nyingine, na hivyo alikuwa na
msaada. Walichokuwa wanakikosa askari wa Sauli ni morali ya vita na waliikosa
kwa sababu kiongozi alikuwa ameacha msingi. Tutazungumza zaidi huko mbele juu
ya kutambua kile kinachokufanya utiwe nguvu, kinachokufanya uwe tofauti, kinachokufanya
utengwe na wenzako na kuonekana wa tofauti. Ukiacha asili ya nguvu zako, huwezi
kupambana vitani na maisha ni vita. Imani ya Israel katika Mungu ndiyo ulikuwa
msingi na asili ya ushindi wa watu vitani. Kama watu hawakuwa wakijua
wanasimama wapi katika mahusiano yao na Mungu, basi hawakuwa na uwezo wa
kupigana na adui. Daudi alikuwa tofauti. Daudi alikuwa na mahusiano thabiti na
Mungu kwa namna yake.
Sikia kauli
yake anaposema “….BWANA aliyeniokoa na makucha ya Simba na makucha ya Dubu,
ataniokoa na Mfilisti huyu…..” Daudi alikuwa na uzoefu si wa vita kwa mfumo wa
kijeshi, lakini kwa vile alikuwa na tumaini ndani ya Mungu, alifahamu kwamba
uzoefu wake ungetumika badala ya ujuzi kwa nafasi hii.
Hakuwa
akitafuta kumpendeza mtu, alikuwa akitafuta kushinda, kutumia yale anayoyajua
kwa ajiri ya kupata hatua mpya katika maisha. Wakati kaka zake walikuwa
wameridhika kutumika kwenye jeshi la Sauli, labda wakirudi nyumbani mara moja
moja na kumletea mzee Yese zawadi kadha, na hata kuwashangaza watu wa kijiji chao kwa mavazi yao ya kijeshI, Daudi
alikuwa na lengo pana zaidi, “….kuifanya jamii yake kuwa huru katika
Israel…….”. Samweli. 17:25 Ahadi ya mfalme kwa yeyote ambaye angemshinda
Mfilisti ilikuwa “…mtu Yule atakayemuua, mfalme atamtajirisha kwa utajiri
mwingi, naye atamwoza binti yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru
katika Israel”. Daudi hakuwa tayari kuacha maneno ya wale ambao waliridhika na
mambo madogo, kumkosesha kile alichoamini Mungu amekiandaa kwa ajiri yake.
Sasa hili
halimaanishi kwamba uwe mkorofi tu na usiyefuata maongozi, lakini inakupasa uwe
na hekima ya kutambua kuna nini nyuma ya kila unachokisikia na kukiona.
Ni kawaida
ya vijana wengi kuwa na ndoto kubwa na mara nyingi tumepita kwenye mambo magumu
yaliyotufanya kufikiri kwamba ikiwa Mungu hakuwa na lengo lolote na maisha
yetu, kwanini ametupitisha kwenye mambo magumu namna hii? Ni sawa kuwaza hivi.
Ndiyo. Kwa sababu kila unachokipitia katika maisha kama kijana, kinakuandaa kwa
kule unakokwenda na utakavyokuwa pindi uwapo mtu mzima.
Ni muhimu
kwa kijana kujitambua. Ingawa kujitambua umekuwa msemo unaotumika sana kwenye
jamii, lakini bado wengi wetu hawafahamu upana wa neno hili na mchango wa
kujitambua kwao katika maisha ya kawaida.
Wako
wanaotafsiri kujitambua kuwa ni uwezo wa kwenda kwa kufuata utamaduni ama
desturi za jamii waishiyo. Japokuwa tafsiri hii inaweza kuwa sehemu ya ukweli,
lakini huu si ukweli wote maana kujitambua ni zaidi ya kutenda kwa namna
inayokufanya kukubalika na jamii yako. Mara nyingi zaidi, kujitambua huweza
kukufanya usikubalike na wengi kwenye jamii yako siyo kwa sababu wanakuchukia,
bali kwa vile wanashindwa kukuelewa na binadamu ni kiumbe mgumu kuishi na mtu
ama kitu asichokielewa.
Kujitambua
ni kufanyaje!?. Nasema kujitambua ni kujihoji na kupata majibu sahihi juu ya
maswali matano kuhusu maisha yako. Maswali hayo ni;
Je wewe ni
Nani!?.
Watu wengi
huamini kwamba wazazi ndiyo wanaokufahamu kuliko mtu mwingine yeyote na hili ni
kweli, lakini wakati wa kuzaliwa kwako yawezekana (hasa kwa vile teknolojia
ilikuwa bado duni) wazazi wako hata hawakujua ikiwa wewe ni mtoto wa kike ama
wa kiume, hawakujua ikiwa una viungo vyako kamili ama una ulemavu fulani,
hawakujua hata uzito wa mwili wako na kadhalika.
Ni vivyo
hawakujua wewe ni nani, kusudi la kuzaliwa kwako ni nini na je utakuja kufanya
nini katika maisha yako!?. Kwao wewe ulikuwa mtu mpya, mtu wa ajabu, na hivyo
walikupa jina kutokana na hisia, imani ama desturi yao tu, walitimiza kwako
wajibu wao kama wazazi wako wa kuhakikisha unapata mahitaji yako ya msingi na
kadhalika huku wakijifunza jambo jipya kuhusu wewe karibu kila siku ya maisha
yako. Ndiyo, walikufundisha mambo mengi, lakini kimsingi hawakuyaweka ama
kuyaumba ndani yako mambo hayo, bali walikusaidia kuyagundua na kuyatumia bila
kuleta madhara kwako na kwa wengine. Ebu fikiri mambo kama kuongea, kusogea,
kutambua sura za watu, mvuto kati yako na watu wa karibu yako, upendo na
kutafsiri matendo ya hisia za upendo kama kutabasamu na kucheka na kadhalika,
mambo haya hukufunzwa na mtu, yalikuwamo ndani yako katika kuumbwa kwako.
Ni kwa uwezo
wa kimaumbile ulitambua matumizi ya viungo mbalimbali katika mwili wako.
Hukusubiri kufundishwa matumizi ya kinywa kwa kula na kuongea, hukusubiri
kufundishwa matumizi ya mikono katika kushika vitu na kadhalika. Pale tu
uliposhindwa kutumia viungo ambavyo ulipaswa kuvitumia bila kufundishwa kufanya
mambo ambayo wazazi wako kwa sababu ya uzoefu walijua unahitaji kuvitumia,
ndipo walipofanya juhudi za utabibu kujua kuna tatizo gani kwamba baadhi ya
viungo havitumiki ama huvitumii na kadhalika.
Hiyo yote ni
kusema hakuna mtu humu duniani anayekujua kama unavyojijua wewe mwenyewe na
hata wewe hujijui kama anavyokujua Mungu muumbaji wako.
Kwa hiyo,
katika kujibu swali la wewe ni nani, kwanza unapaswa kuondokana na tafsiri za
watu kuhusu wewe ni nani. Wakati Yesu alipoanza kusema na kufundisha, viongozi
na hata watu wengine katika jamii yake walianza kutafuta kumfungia kwenye upana
wa vile walivyokuwa wakimuona na hivyo si ajabu waliuliza; “…….huyu si mwana wa Seremala……..
na nduguze tunao hapa kwetu……….!?
Katika hatua
hii ya kujitambua kama kijana kwa kujitafsiri wewe ni nani, inakupasa
kujihadhari usijifungie kwenye tafsiri za watu waliokuzunguka.
Huwezi
kutambua kusudi ama uwezo wa mashine yoyote bila kwanza kumsikiliza
mtengenezaji wa mashine husika ama kusoma maelekezo yake kuhusu mashine hiyo.
Vivyo wewe, huwezi kuutambua uwezo wako, vipawa vyako, mipaka yako na kadhalika
isipokuwa utambuzi huo unatoka kwa mtengenezaji ama muumbaji wa wanadamu naye
ni Mungu. Ndiyo maana mwandishi wa Zaburi anasema “…..kwa kutii akilifuata neno
lako”
Pengine
unawaza kama yule kijana tajiri aliyemwambia Yesu “…..hayo yote nayajua na
kuyafuata tangu ujana wangu….”. Uko sahihi, na ndiyo maana si lengo langu
kukupa majibu ya moja kwa moja juu ya swali hili. Naweza kukwambia walau kwa
usahihi wa kiwango fulani kwamba mimi ni nani, lakini siwezi kukwambia wewe ni
nani. Ninaweza hata hivyo kukushawishi ujiulize swali hili kwa sababu ni muhimu
sana. Ni swali ambalo litakufanya utafiti na kuhoji kila kitu kuhusu wewe, ni
swali litakalokufanya uchunguze madhaifu yako na mazuri yako na kuyaweka yote
kwenye mizani katika kutafuta majibu, na ni katika kufanya hivyo tu,
unapoboresha uwezo wako wa kujipambanua na hivyo kujitambua.
Ebu fikiri
kwamba wakati ninapoandika maandishi haya, idadi ya watu duniani inafikia watu
bilioni saba na kila mtu anavyo vitu kwenye vinasaba (DNA) vyake
vinavyomtofautisha na mwingine. Alama zako za vidole hazifanani na za mtu
yeyote yule duniani, mboni zako za macho zina tofauti na watu wengine wote
duniani na hata mvumo wa sauti yako ni tofauti na watu wengine wote duniani.
Hii maana yake ni kwamba wewe ni mtu tofauti na watu wengine wote waliowahi
kuishi, wanaoishi na watakaoishi baada yako. Wewe ni maalumu sana. Tafuta
kuutambua umaalumu wako. Inaaminika kwamba ujuzi sahihi huja kwa kuuliza
maswali sahihi na mimi naamini pia katika kuuliza mahala sahihi, na majibu ya
wewe ni nani yanaweza kutolewa na Mungu muumbaji peke yake.
Hiyo
haikuzuii hata hivyo kujisomea vitabu na tafiti kadhaa kuhusu watu wa aina yako
hasa kwa sababu Kwanini ni swali ambalo limekuwapo kwa miaka dahali na
litaendelea kuwapo. Sijaribu kukushawishi ujisomee Biblia ama vitabu na
machapisho ya dini peke yake, maana kwa kufanya hivyo utakuwa umeshindwa
kuyashindanisha mawazo na kushindanisha mawazo ndiyo hulka bora kabisa ya
binadamu.
Ninakushawishi
ujisomee na kutafiti kwa kadri unavyoweza na kujiongezea maarifa katika
kujitafakari, kuvumbua hazina za vipawa na karama vilivyomo ndani yako,
kutafiti mahala na wakati unapoweza kutumia vipawa hivyo na kadhalika, lakini
nakushauri ufanye hivyo ukiwa na msingi kwenye neno la Mungu maana kama ilivyo
kwamba kila chombo kilichoundwa na mwanadamu kimeandikiwa namna ya matumizi
yake, kadhalika Mungu ameandika kuhusu uumbaji wake na masharti ya matumizi
yake. Tunapokiuka, tunatafuta madhara.
Inaendelea......!
Inaendelea......!
No comments:
Post a Comment