Ni kama mara nyingine Mungu hutumia mambo mabaya
yanayotutokea kwenye maisha ili kutonyesha wito wetu hasa na kutuongoza kule
ambako alitukusudia tangu kuwekwa misingi ya nchi. Tukiungana na Muhubiri
kusema “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya
mbingu”,(Mhubiri 3:1) tunapaswa kujifunza pia kwamba kuna changamoto zitokanazo
na mabadiliko ya wakati na majira kwenye maisha yetu.
Moja ya changamoto ambazo zimenikabili mimi binafsi
katika maisha yangu, ni kuvitambua na kuishi kwenye vipindi vya mpito. Kwa
sababu mimi ni mtu ambaye nimeishi aina nyingi za maisha, nimejifunza kwamba
mara nyingi wakati tunapokuwa hatuna jinsi yoyote isipokuwa kutumaini katika
Mungu, huo ni wakati mgumu sana kwetu. Lakini huo ni wakati mzuri pia kwetu kwa
sababu hutusaidia kuonyesha uwezo wa utu wetu. Mara nyingi nimejua moyoni
mwangu kwamba hali ya mazingira ama mahusiano inaanza kubadilika hapa nilipo na
kwamba ni wakati wa kwenda hatua nyingine, lakini hofu yangu ya kuacha kile
nilichokizoea, kubadili lile ambalo ni kawaida na kuchukua hatua kwenye
sintofahamu, kwangu hiyo huwa changamoto kubwa. Binafsi nimekuwa nikilazimishwa
na Mungu kubadilika na usidhani imekuwa rahisi hasa wakati wa mchakato husika.
Haikuwa rahisi kwa Musa. Kwanza alikuwa mtu aliyeishi kati ya mawazo mawili kwa
muda mrefu sana, na alikuwa na utambulisho usioeleweka. Usingemtanabahisha kama
Mmisri kwa sababu hakuwa Mmisri kwa kuzaliwa na bila shaka katika maisha yake
ya kila siku alikuwa akiambiwa kwamba kama siyo tu kufadhiliwa na binti Farao,
basi angekuwa huko Gosheni akifyatua matofali na Waebrania wenzie.
Ni ajabu lakini ukweli mchungu kwamba watu watakupokea
kwenye kariba yao kama hawana budi isipokuwa wanalazimishwa kukupokea, lakini
hawatakuacha kusahau wewe ni nani. Watatumia kila nafasi waipatayo kukumbusha
kwamba hukustahili kuwa hapo, watatumia kila mapungufu yako kukusimanga na
kukufanya ujisikie mnyonge, japo kwa wasiojua watakuona kuwa mtu mwenye furaha
sana lakini siri ya moyo wako unaijua mwenyewe.
Nakumbuka jinsi nilivyoishi kwa shida kwenye nyumba ya
mmoja wa ndugu zetu aliyekuwa mtu mkubwa na kiongozi wa serikali wakati huo.
Nilikuwa nimetoka kijijini kwa ajiri ya kusoma eneo la mjini ambako mama yangu
alikuwa akifanya kazi, lakini kwa sababu ya udogo wa nyumba aliyokuwa akiishi
mama yangu, mimi nililazimika kwenda kuishi kwa huyo ndugu. Nilikuwa darasa la
tatu na pale nyumbani kulikuwa na watoto wa darasa langu na wengine wakubwa
kidogo. Wakati wa kula, mimi nilipaswa kusubiri kwanza wao wamalize kula ndipo
na mimi nile. Sikuweza kula baadhi ya vyakula ambavyo vilihesabiwa kuwa vya anasa
kama maziwa, juisi, nyama na kadhalika isipokuwa mara chache tu ikiwa mwenye
nyumba alikuwampo, ambapo nilipata pia nafasi ya kukaa na familia nzima
sebuleni kwa ajiri ya chakula na kutazama televisheni.
Kama mwenye nyumba hakuwapo, na kwa sababu ya kazi na
nafasi yake alikuwa akisafiri sana, niliishi kila sekunde kama mtumwa, kila
mara nikikumbushwa kwamba nilikuwa mshamba niliyetoka kijijini na nisiyestahili
kutangamana na wao. Mambo hayo pamoja na kwamba yaliniumiza moyo, lakini
yamenifanya kuwa makini na watu ambao Mungu ananipa nafasi ya kuwasaidia kwa
lolote, nimemwomba Mungu anipe neema nisiseme lolote la kuwatweza maana nayajua
maumivu yake. Nimejifunza kwamba watu hatuwezi kufanana kufikiri na kutenda
kwetu na hivyo ikiwa tunaishi pamoja, basi kumbe itatupasa kuvumiliana sana.
Naona kama Musa naye alikuwa na wakati wa namna hii.
Wanahistoria wa utawala wa Misri wa wakati huo wanasema baada ya kifo cha
Farao, mmoja wa wana wa mfalme angeweza kuchukua nafasi ya kuwa Farao wa Misri.
Hili nalo bila shaka liliongeza shida kwa Musa hasa kwa vile baadhi ya
wanahistoria wanasema Musa alikuwa na uwezo maalumu katika mapigano na busara
ya utawala kuliko wenzake na hivyo alipopata tuhuma ya kuua mtu, tena kutoka
kwa watu wake mwenyewe, sasa alikuwa na wakati mgumu zaidi, adui zake walikuwa
wamepata sababu ya kumshambulia zaidi. Lakini pia yasemekana Farao Tuthmosis II
alimpenda Musa na sasa alikuwa njia panda. Si ajabu ambavyo hata waliokuwa
rafiki zako kwenye mamlaka hugeuka kuwa adui zako wakati wa kujiliwa kwako
ukifika!?. Si ajabu kwamba sifa ileile iliyokufanya kuajiriwa, ndiyo sifa hiyo
hiyo inayokufanya leo wanatafuta kukuaa!?. Kwani si ujuzi wa mapigano na uwezo
wa maamuzi wa Musa uliokuwa umempa sifa mbele ya Farao, lakini haki ilipodai
kwamba Mmisri ashughulikiwe kwa uwezo ule ule, moto ukawaka na Musa akajikuta
hana kwao?.
Tambua Changamoto za wakati wako au kwa kusema sahihi,
tafuta wakati wako ndani ya changamoto zako maana Mungu hataruhusu jambo
litokee kwako ambalo hujaweza kukabiliana nalo. Huu ulikuwa wakati wa Musa
kusogea hatua nyingine na hii haikuwa hatua nzuri sana kwa Musa lakini ilikuwa
sahihi, ya lazima kwa ajiri ya kusudi la Mungu. Kutoka Ikulu hadi katika Jangwa
la Moabu, mwana wa mfalme aliyegeuka mchunga mbuzi. Bila shaka Wamisri wangecheka
sana kwa kusikia habari hizi. Lakini ni kipawa chake hiki hiki cha maamuzi,
moyo wa kupenda kuona haki, moyo wa kutoona wanyonge wakionewa, ndivyo
vilivyomfikisha kwa Yethro. Ni vipawa vyake hivi hivi vilivyoendelea
kumtengenezea njia hata kwenye hatua hii. Mapenzi yake ya kuona haki
inatendeka.
Kut 3: 16-22 “Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti
saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi
la baba yao. Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia,
akalinywesha kundi lao. Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea
mapema leo? Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji,
tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi?
Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula. Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti
yake, Sipora. Huyo akamzalia mwana, akamwita jina lake Gershomu, maana
alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni”.
Tukutane kwenye sehemu tatu za mwisho katika sura hii ya kwanza kuanzia juma lijalo.