Saturday, September 7, 2013

Wakati wa Kujaribiwa: Sehemu ya Kwanza.



Biblia inaeleza wazi kwamba kuna “…wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu” Muhubiri 3:1. Ukilisoma andiko hili na kutazama hali ya maisha ya kila siku ya Ukristo, utagundua kwamba kuna wakati maalumu wa kujaribiwa. Luka 22:52-53, Bwana Yesu anawaambia wale waliokuja kumkamata kwa nini hawakuwa na wazo la kufanya hivyo hapo kabla, na anasema ni kwa sababu wakati wao ulikuwa bado. Ukipata nafasi ya kujifunza somo liitwalo “Majira na nyakati za mkristo” utaelewa zaidi kuhusu majira na wakati katika maeneo tofauti ya maisha ya mkristo wakati anaposafiri kwenda mbinguni lakini kwenye somo hili tunaangazia mambo kadhaa kama ifuatavyo:
(1)  Jaribu ni nini?
Watu wengi wamekuwa na tafsiri tofauti kuhusu jaribu, lakini si zote zilizo sahihi kwa mujibu wa maandiko. Wengi wa watu wa Mungu huita kila tatizo au changamoto wanayokutana nayo kwenye maisha kuwa ni jaribu. Tafsri hii si sahihi kwa mujibu wa maandiko. Ebu tazama jinsi ambavyo Biblia inayatofautisha matatizo mengine ya kimaisha na majaribu ya kiimani.
 Jaribu ni kipimo cha Imani. Ebu tuseme jaribu ni mtihani wa imani, maandiko hutuonyesha kwamba Imani huja kwa (hutokana na) kusikia (au kujifunza) neno la Kristo (Warumi 10:17) na hivyo baada ya kuwa umeingia kwenye darasa la imani na kujifunza mambo kadhaa wa kadhaa, huitajika ufanye mtihani ambao siyo tu hupima kiwango cha uelewa wako, lakini huamua ikiwa uko tayari kwa kiwango kingine au bado, maana tunatoka imani hata imani hata tukifikie kimo chake Kristo. Warumi 1:17. Hivyo mengi ya yale tuyaitayo matatizo kwenye maisha yetu kama wafuasi, ni mchakato wa kusogea hatua nyingine zaidi.

Mwanzo 22:1 “Baada ya mambo hayo , Mungu alimjaribu Abrahamu….” Tazama msitari huu unavyoanza kwa kusema ‘baada ya mambo hayo’, ndiyo kusema palikuwa na mambo kadhaa yaliyokuwa yametokea kabla ya Abrahamu kujaribiwa. Ni ngumu kueleweka kwa akili za kibinadamu kwamba baada ya Mungu kuwa amemwita Abrahamu kwenye sura ya 12 ya kitabu cha Mwanzo na Abrahamu akatii, baada ya Mungu kumpa Abrahamu ahadi ya uzao mwingi kwenye sura ya 13,  baada ya Mungu kumpigania Abrahamu kwenye sura ya 14 na Abrahamu kumtolea Mungu fungu la kumi kupitia kwa Melkizedeki, baada ya Mungu kumhakikishia Abrahamu kwamba uzao wake mwenyewe ndiyo utakaomrithi na  hapa naomba niseme wazi kwamba Mungu kumhakikishia Ibrahimu juu ya kurithiwa na uzao wake mwenyewe alikuwa amejibu moja ya vitendawili vikubwa vilivyokuwa vikimkabili Ibrahimu, unaweza kumuona Ibrahim akijaribu ‘kumshawishi’ Mungu akubaliane na Ishmael kuwa mwana wa ahadi kwenye Mwanzo 17:17. Ni kama Ibrahimu anamwambia Mungu “ Unajua hili suala linanishinda hata kulielewa, kwa nini tusimalize tu hili jambo kwa kumtwaa Ishmael awe mwana wa ahadi?”. Jibu la Mungu kwa Ibrahim lilikuwa  kumpa Ibrahim jina la mtoto na “…kwa habari ya Ishmael nimekusikia…..”. Ni kama Mungu akisema, Sawa Ibrahim rafiki yangu, ninaelewa kwamba linakusumbua na kwamba unampenda pia mwanao Ishamel,  “…nimembariki…..”.
 Ndiyo maana Roho Mtakatifu anatuwekea jambo hili kwenye maandiko anaposema “Baada ya mambo hayo, Mungu alimjaribu Ibrahim……” Ibrahim alikuwa ametembea na Mungu ya kutosha kujifunza kwamba Mungu anajari mpaka yale mambo madogo madogo yatuumizayo kwa ndani sana. Yale ambayo hatuna hata maneno ama ujasiri wa kutosha kuyasema mbele za Mungu. Mambo ambayo hatuna hakika kama Mungu mkuu namna hii angependa kusikia hoja hizi kutoka kwetu. Pana nyakati katika maisha ambapo tunajaribu kuwaza kwamba Mungu hajari chochote kuhusu hisia zetu isipokuwa  mapenzi yake tu yatimizwe, basi!. Ibrahim alikuwa amejifunza kwamba Mungu alikuwa si dikteta anayetoa tu amri na mipango yake kwenye maisha yetu, bali Mungu anayejari na ambaye anafanya mambo kutubariki. Ibrahim alikuwa amepata daraja flani la Imani na Baraka na sasa ilikuwa wakati wa Ibrahim kusonga mbele tena.

  Sura ya 22, tunamuona Mungu akimjaribu Abrahamu.  Hapa tunaona mambo mawili makubwa. Moja ni kwamba tangu Abrahamu kuitwa asijue aendako (Waebr 11:8) hadi kupigana vita vya kumkomboa ndugu yake (Mwanz 14:13-16) na hata suala la Abrahamu kukosa mtoto kwa miaka mingi, hayo hayakuwa majaribu, na kama yalikuwa majaribu basi hakujaribiwa na Mungu. Maana Biblia inayaweka kwenye fungu moja ambalo Biblia inaliita “Baada ya mambo hayo…” na ndipo inasema Abrahamu alijaribiwa. Pili ni kwamba katika mambo yote hayo ambayo Abrahamu alikutana nayo, Imani yake haikuwekwa njia panda, haikujaribiwa na ndiposa kila anapovuka hatua flani utamuona Mungu ama akilithibitisha tu agano lake kwa Abrahamu au akitoa maelekezo flani, lakini anapovuka kwenye jaribu unaona Mungu akisema jambo tofauti (Mwanzo 22:12) anasema “…sasa najua kwamba unamcha Bwana…”. Maana yake maelekezo ya Mungu mara hii yaliilenga imani ya Abrahamu na siyo kitu kingine.

Ebu fikiri kwenye maisha yako binafsi, wakati ambapo mawazo yako yanakuambia sasa uko sawa  mbele za Mungu na moyo wako ukitegemea kuona Baraka za Mungu, ndipo wakati huo unapojaribiwa.  Tunasoma kitu kinachofanana na hiki kwenye habari za Yusufu, Mwanzo: 39:1-6b. Kwenye maandiko haya utamuona Yusufu akibarikiwa na kupata kibali japokuwa alikuwa  ameuzwa. Aliachiwa kila kitu na bwana wake hata bwana wake “hakujua habari ya kitu chochote chake, ila hicho chakula alichokula” na mstari wa saba unaanza kwa neno hili “Baada ya mambo hayo….” Maana yake baada ya Mungu kuwa amemuonekania Yusufu namna hii, ulikuwa umefika sasa wakati wa Yusufu kujaribiwa.  Utagundua jinsi ambavyo Yusufu alipitia mambo mbalimbali na si mambo yote hayo yalikuwa majaribu. Utaona jinsi ambavyo Yusufu hakuwa na hofu ya “kumkosa Mungu” katika mambo yote aliyopitia  isipokuwa suala la mke wa Potifa lilitishia mahusiano yake na Mungu, lilimuweka njia panda  ikiwa aamue kutembea na mke wa bosi wake (angepata unafuu flani katika maisha kwa kipindi flani) au amuheshimu Mungu halafu aingie kwenye ugomvi na huyu mama kwa vile kwa vyovyote mke wa Bosi wake angejutia kitendo cha kuzifunua hisia zake kwa mtumishi wake na hivyo angekasirika na Yusufu yamkini alifahamu hivyo.  

Tofauti kati ya Jaribu, Kwazo na Teso.
Labda si rahisi sana kuelezea jaribu vizuri kwa kulitofautisha na magumu mengine tuyapatayo katika maisha hata hivyo hapa chini tutajaribu kutofautisha kati ya Jaribu, Kwazo na Teso kwa sifa za mambo haya matatu.
 Jaribu huilenga imani yako yaani mahusiano yako na Mungu moja kwa moja (Ayubu 1:9) kwa kuleta mambo katika maisha yako ambayo ama yatakufanya umtilie shaka Mungu na ahadi zake, utayari au hata uwezo wa Mungu kuzitekeleza, uhalali wa amri za Mungu kwenye maisha yako na kadhalika. Ona jinsi ambavyo shetani hapa hana shida na mali za Ayubu, bali ni kama anamwambia Mungu, “Nahisi Ayubu anakuheshimu kwa ajiri ya  baraka ulizompa na nina uhakika ukimyang’anya basi atahamia kwenye kambi pinzani na wewe”. Ndiyo maana anasema “…naye atakukufuru mbele ya uso wako” Ona ambavyo Mungu hana mashaka na imani ya Ayubu lakini anamruhusu shetani kwenda na kumjaribu kwenye mali zake zote. Twaweza kujifunza mengi kwenye majaribu ya Ayubu kama tutakavyoona huko mbeleni.
 Kwazo huilenga akili yako kwa kutokeza mambo ambayo ama hayakubaliani na falsafa ama misimamo yako mingineyo katika maisha. Ndiposa Yesu Kristo anawaambia wanafunzi wake kwamba “…makwazo hayana budi kuja…” Luka 17:1-3. anawaambia makwazo ni matokeo ya makosa ya kutokufahamu jinsi ya kuyaweka pamoja mazuri na madhaifu yetu katika maisha na hivyo mara nyingi twakoseana na kughafirishana. Na hivyo mwokozi anatushauri  “…jilindeni, kama ndugu yako akikosa, muonye, akitubu msamehe”. Shida kubwa zilizoko leo, zisingekuwako kama tungejifunza juu ya  kuzungumza na  waamini wenzetu kanisani, wafanyakazi wenzetu mahala pa kazi na hata wenzi wetu kwenye ndoa na familia juu ya mambo ambayo tunadhani hayakuwa sawa walipoyasema ama kuyatenda, tujaribu kuwasikiliza wanapotupa sababu za wao kutenda au kusema hivyo na kwa upendo tuwaonyeshe makosa yao. Hapo bila shaka watatubu na sisi tutawasamehe na makwazo yatakomea hapo. Ni vivyo tunapowakosa wenzetu na wakatueleza makosa yetu, tunatubu na kuwaomba watusamehe na makwazo yanakomea hapo. Ebu tazama Lutu na Abrahamu walivyokwazana na wakamaliza tatizo lao kwa mazungumzo. Mwanzo 12:1-12.

1Sam 30: 1-6 .Habari za Daudi kwenye sura hii zaweza kutufunza vizuri juu ya hili, Daudi na kikosi cha askari wake 600 walikuwa wamekimbilia Gathi ili wakae mbali na Sauli. Inaonekana mfalme wa Gathi alikuwa akimuunga mkono Daudi na hivyo alikuwa amempa mji mmojawapo ili yeye na watu wake waweze kuishi.
Siku moja vita vikalipuka kati ya mfalme wa Gathi na Israel na Daudi akitaka kurudisha fadhila kwa mwenyeji wake akaamua kwenda na jeshi lake kwa ajiri ya kupigana dhidi ya Israel, lakini kwa sababu za kiusalama, washauri wa masuala ya usalama wa serikali ya Gathi hawakutaka Daudi aende nao vitani na hivyo akaruhusiwa kurudi yeye na jeshi lake kwenye mji wao. Walipofika, siyo tu mji haukuwepo bali hata familia ya Daudi na familia za askari wake hazikuwapo, maadui walikuwa wameuvamia mji wakauchoma moto na kuwachukua mateka watu wote na pia kuzichukua mali zote kuwa nyara. Biblia haisemi ni kwa nini hawakuwaua watu wote kama ilivyokuwa desturi ya vita, labda kwa sababu walikuwa hawakukutana na upinzani wowote kwa vile askari hawakumo kwenye mji au lah! Lakini ni vyema kusema, Mungu alikuwa amewaponya watu hawa na kuwalinda wasiuawe na adui. Askari wa Daudi kwa mara ya kwanza wakatishia kuasi, walitaka kumpiga mawe kiongozi wao ambaye wamempenda na kumfuata miaka yote. Wengi wa askari hao walikuwa kwa hiyari yao wenyewe wamemfuata Daudi huko msituni na kujiunga naye wakiwa wameacha nyuma maisha yao ya kawaida kwa hiyari yao, lakini hili lilikuwa nimewakasirisha sana na japo halikuwa kosa la Daudi kwa kile ambacho kinaelezwa kwamba “…kwa kuwa nafsi za hao watu zilighafilika sana….”(KJV). kwa tafsiri nyingine watu hawa walikuwa wamekasirika ama kukwaza, lakini siyo kujaribiwa.

Twaweza pia  kusema, kwazo linalenga  furaha na amani ya moyo. Zab 119:165. Tafsiri ya neno “kuwakwaza” kwenye kiingereza (KJV) inasema “to offend them” inatumia neno ‘offend’  ambalo tafsiri yake ni ‘kosea’ ama ‘umiza kihisia’ ‘finya’ na ambalo linatokana na neno “offense” yaani kosa.

Kwa hiyo makwazo Ni mwitikio wetu Kwa makosa ama yetu wenyewe, au ya wenzetu na matokeo yake kwenye maisha yetu ya kila siku.   
 Teso  ni hali ambayo huruhusiwa kwa upendo na Mungu kwenye maisha yetu kwa ajiri ya kukomesha mambo fulani yasiyopendeza katika maisha yetu. Hii ni ajabu kwamba katika upendo wake, muumbaji wa vitu vyote humtumia mwanadamu teso fulani katika maisha yake ili asiingie katika njia isiyompasa. Zab 119:71, Ayubu 36: 15, Zab  118 :18  . Pia  Mungu huyatumia mateso kututendea kama wana wa Mungu na ni kwa faida yetu wenyewe Ebr 12:10. Pia Mungu hutumia teso kama njia ya kuwafundisha watu (hata wale ambao sio wanaoteswa) juu ya jambo flani la Kimungu Daniel 4-5
Kwa hiyo tumeona mambo kadhaa yanayotofautisha jaribu na changamoto nyingine tuzipatazo katika maisha.
(i)              Kwanza jaribu lina muda wake
(ii)            Pili jaribu linalenga imani yako katika Mungu moja kwa moja
(iii)          Tatu jaribu huja baada ya kuwa  Mungu amejifunua kwa jinsi flani kwako.   
 Tutazungumza suala la Muda wa jaribu huko mbeleni kwa upana zaidi.
  * Kwa hiyo twaweza kusema, Shida (changamoto) yoyote haiwi jaribu hadi imekuweka njia panda, uchague kati ya kumtii Mungu au kuchukua maamuzi mbadala yatakayokuepusha na shida inayokukabili. Mwanzo 39:9b, Daniel 3:14-18, Ayubu 2:9-10, 1Pet 1:7

No comments:

Post a Comment