(1) Aina
za Majaribu
Majaribu yote hayako kwenye kundi
moja tu. Ziko aina kadhaa za majaribu na hapa tutataja aina kuu tatu za
majaribu ambazo ni:
(i)
Majaribu yatokanayo na Tamaa binafsi za mjaribiwa.
Hii ni aina ya majaribu ambayo
mjaribu anategemea hali na mazingira yetu kabla hajatujaribu. Yak 1:12- 14.
Pamekuwa na makosa ya tafsiri
kuhusu andiko hili ambalo mzee Yohana anatuandikia kutuonya juu ya kujaribiwa
na tamaa zetu. Watafsiri wengi wamelifanya neno hili kuwa kwamba tamaa
alizozimaanisha Yakobo hapa ni tamaa mbaya tu. Lakini ni vyema kudiriki
kutafakari zaidi kidogo ya hapo na kufikiri kwamba yawezekana si tu tamaa mbaya
huwajaribu watu bali hata tamaa nzuri. Ebu fikiri unapotamani kuendesha gari zuri
kama la mtu fulani unayemuona kila unapokwenda
kazini. Hii bila shaka ni tamaa ya maendeleo na imeumbwa hivyo moyoni mwa
binadamu na Mungu mwenyewe kwa ajiri ya kukusaidia ukue na kuongezeka. Lakini
mara adui shetani anapogundua juu ya tamaa yako hiyo, yeye hukuletea mawazoni kwako njia ambazo waweza
kuzitumia kujipatia gari la jinsi hiyo na hata bora kuliko hilo na mara zote njia ambazo ukuonyesha si
za halali bali ni zile ambazo ni kinyume na neno takatifu la Mungu. Ndiposa Yakobo anasema “…huku akivutwa…”
maana yake kuna mahala huyu mtu mwenye tamaa amesimama na kuna nguvu inayomvuta
kutoka hapo. “…na kudanganywa..” hii ni kusema yeye aliye baba wa uongo huingia
kazini kumdanganya mtu huyu ama akitumia watu walio upande wake au
akiyashambulia mawazo yake moja kwa moja. Mathayo 4: 2-3. “….mwisho akaona
njaa. Mjaribu akamjia…” hapa unaweza kuona jinsi mjaribu alivyochukua hadhari
kubwa kusubiri Yesu aone njaa na ndipo akamjia. Wote tunajua kwamba baada ya
kufunga kwa siku arobaini, Yesu alikuwa na haki kabisa kuona njaa ila shetani
alitaka kuutumia mwanya huo kumtegenezea njia ya mkato katika kufikia hitaji
lake la kupata chakula na njia hiyo ya mkato ingekuwa dhambi mbele za Mungu.
(ii)
Majaribu
yatokanayo na shetani
Hii ni aina ya majaribu ambayo
shetani moja kwa moja anakushambulia kwa lengo la kukutoa kwenye msimamo wako
kwa Mungu wako. Bila shaka hii ni aina ambayo imewakumba na kuwaua wengi
kiroho. Mathayo 4:8-10 hapa tunamuona
Ibilisi akimjaribu yesu kwenye eneo ambalo Ibilisi mwenyewe na Yesu wanajua
kwamba haipaswi kwa mwanadamu kumsujudia mwingine yeyote isipokuwa Mungu peke
yake. Ibilisi anatumia mali,
mamlaka, hata umaarufu kumshawishi Yesu kwenda kinyume na maagizo ya msingi ya
Mungu kwenye uumbaji wake. Kwenye maeneo mengi ya maisha yetu ya Ukristo
tumeshindwa kusimamia kweli ile tunayoifahamu kwa ajiri tu ya kupata faida
flani ya kidunia na ni hapo shetani alipopata nafasi ya kujitukuza juu ya imani
zetu. Fikiri ni wakristo wangapi wameacha misingi ya imani yao
kama kufunga na kuomba, kuhudhuria ibada na
kadhalika kwa sababu muda huo ni muhimu kwa ajiri ya kufanya shughuli nyingine
za kujiongezea kipato. Katika dunia inayoendelea kwa kasi hivi, hali hii
huonekana ya kawaida, lakini maandiko yametuonya kabla (Mark 4:19). Kama kuna shida kubwa inayolikabili kanisa kwa ujumla
wake na kila mwamini mmoja mmoja ni
kuenenda kwa kawaida ya dunia yaani kusema ni kawaida kwa mambo ambayo dunia
husema ni ya kawaida. Vijana wangapi wanafanya kile ambacho Biblia huita
uasherati kwa vile ( kwa tafsiri ya kidunia) ni kawaida kwa kijana kuwa na
mpenzi wake mradi tu asiwe na zaidi ya mpenzi mmoja kwa wakati mmoja?.
Njia ya pili ambayo shetani
amekuwa akiitumia katika kuwajaribu watu ni kwa kutumia dhiki na mateso. Njia
hii ilikuwako tangu zamani hata hivyo si mpya Dan 3: 13-23. Ebu waza juu ya
vijana watatu ambao kwanza wanaishi uhamishoni kwa sababu ya hali ya kukosekana
usalama nchini kwao. Hali hii inaweza isieleweke kwa nchi zile ambazo
hazijashuhudia vita hata vya wenyewe kwa wenyewe, lakini kwa nchi ambazo
zimepitia uzoefu huu, watu wake wanajua jinsi ilivyo vigumu kutunza utamaduni
wenu mkiwa ukimbizini. Taifa la Israel
ni taifa ambalo utamaduni wao ulifungwa kwenye Torati na ambayo ilikataza si tu
kusujudia sanamu, bali hata kuzitengeneza kwa lengo hilo. Kumb 5:8-10 hapa sasa imejitokeza hali
ambayo vijana hawa wanatakiwa kuamua, ikiwa wayatunze maagizo ya Mungu ama
wajiokoe na kifo cha kuchomwa moto? Ufunuo 2:10-11.
Yako maeneo mengine ambayo twaweza
kujifunza juu ya majaribu yatokanayo na shetani, lakini ni vyema hapa uone
tofauti ya msingi iliyoko kati ya jaribu na jaribu kwa vile hi ni sehemu muhimu
katika kushinda jaribu lako.
Pana jambo ambalo nafikiri
niliweke vizuri hapa, kwenye maisha yetu kama wakrsito, nguvu au falme mbili
zinashindana katika kutaka kuchukua nafasi ya kwanza kwenye maisha yetu nazo ni
ufalme wa giza
na ufalme wa nuru. Hivyo ni vyema kufahamu kwamba kila kitu kinachotokea kwenye
maisha yako, ufalme wa giza
hujaribu kukitumia katika kukuhamisha kutoka ufalme wa nuru. Ashukuriwe Mungu
ambaye hufanya kazi katika mambo yote katika kuwapatia mema wale wampendao.
Ni muhimu hata hivyo kufahamu
kwamba pana tofauti wakati shetani anapojaribu kutumia tamaa zako mwenyewe
kukuondoa katika mahusiano yako na
Mungu, hapo ndipo unapojaribiwa kwa tamaa zako mwenyewe. Wakati shetani anapokukabili moja
kwa moja na kukutaka ufanye maamuzi ya kumfuata (kumwabudu), hapo ndipo
unapojaribiwa na shetani. Japo shetani ndiye hutujaribu pia wakati
tamaa zetu zinapohusika.
Pana nyakati pia ambapo shetani
hutushawishi kutumia nafasi ama vipaji vyetu katika maisha kufanya jambo ambalo
siyo tu litakuwa kinyume na mapenzi au maelekezo ya Mungu kwenye maisha yetu,
bali pia jambo hilo
ama litakinzana na sheria za nchi au sheria zinazosimamia nafasi tulizo nazo
katika jamii. Mathayo 4:5-7. 1 Sam 24:1-7. Daudi alipata mara mbili
nafasi ya kumuua adui yake Sauli ambaye ndiye hasa alikuwa kikwazo cha Daudi
kuwa mfalme kama alivyokuwa ametabiriwa na
Samweli. Kwa mtizamo wa kawaida, Daudi alipaswa kumpiga Sauli na kumuua na
kisha kutafuta njia yake kwenye ikulu ya Israel, lakini Daudi aliugundua
haraka mtego wa shetani uliokuwa mwenye kitendo cha Sauli kuingia kwenye
mavizio yake. Kulikuwa na sheria iliyokataza mtu yeyote kwa sababu yoyote
kumtendea kwa hila mpakwa mafuta wa Bwana, na hapa shetani alikuwa
akimwekea Daudi njia rahisi ya kufikia
kusudi la yeye kuwa mfalme. Tunasoma “…nao
watu wa Daudi wakamwambia , Tazama , hii ndiyo siku ili aliyokuambia Bwana,
Angalia, nitamtia adui yako mkononi mwako, nawe utamtenda yoyote utakayoona
kuwa mema”. (1 Sam 24:4). Kumbuka kwamba Daudi alikuwa akiongoza kile
ambacho wanasiasa wa karne ya ishirini na moja wangekiita jeshi la waasi, na hapa wawili labda watano
wa makamanda wake, bila shaka ambao waliweza kuongea na kumshauri Daudi,
wanampa ushauri sahihi kwa mujibu wa hali halisi ya kisiasa na labda ya kijeshi
na kivita lakini siyo kiroho.
Jambo hili linajitokeza tena mara
ya pili, 1 Sam 26: 5- 12 na unaona jinsi ambavyo Daudi anaendelea kusimamia
imani yake zaidi ya uhalisia wa mazingira yanayomkabili kwa wakati huo. “Ndipo
Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako mkononi mwako leo, basi,
niache nimpige kwa hilo
fumo hata nchi kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili. Lakini Daudi akamwambia
Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya
masihi wa Bwana na asiwe na hatia?” 1Sam 26: 8-9.
Ona ambavyo hata katika huduma ya
kanisa twaweza kujaribiwa kuipita mipaka tuliyowekewa na kutaka kufanya huduma
zote sisi kinyume na agizo la Mungu. 2 Nyakati 26:16-20. Uzia, mfalme ambaye
alikuwa amesimama na Mungu kwa sehemu kubwa ya utawala wake, alikuwa ameshindwa
kuigundua mbinu ya shetani hata akajikuta ameongozwa na kiburi cha kuwadharau
wengine kwenye taifa la Mungu kwa wito wao na kuingia hekaluni kufukiza uvumba.
Mungu akampiga kwa ukoma.
(iii) Majaribu
yatokanayo na Mungu.
Wakristo wengi huamini kwamba
Mungu huwa hamjaribu mtu, Uko pia mstari wa Biblia ambao ni kama
unaunga mkono mtizamo huo. Yak 1:13 “Mtu ajaribiwapo asiseme, Ninajaribiwa na
Mungu; …” Watu wengi wameuchukua mstari huu na kudai Mungu huwa hamjaribu mtu
bila kusoma sehemu ya mwisho ya mstari huu isemayo “…maana Mungu hawezi
kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu” Hii ni kusema, kuna
jinsi ambavyo Mungu aweza kumjaribu mtu isispokuwa siyo kwa maovu.
Mwanzo 22: 1 husema juu ya Mungu
kumjaribu Abrahamu inaposema “Baada ya mambo hayo, Mungu alimjaribu Abrahamu…” Hii
ni kusema Mungu humjaribu mtu kwa sababu na njia tofauti kila mara lakini kwa nia
na lengo jema. Majaribu yatokanayo na Mungu huwa na sifa tofauti na majaribu
mengine kwa sababu hulenga zaidi kuboresha mahusiano yetu na Mungu na mara zote
yana lengo la kutufaidia wenyewe au jamii yetu. Kwa kusema kwa usahihi ni kwamba Mungu huruhusu
kujaribiwa kwetu kwa kuboresha mahusiano yetu naye na kutufaidisha sisi moja
kwa moja ama kwa kutufanya msaada kwa jamii yetu na hivyo kupata ridhiko la
ushiriki wetu kwenye maendeleo au faida flani ya jamii yetu. Ni aibu kwamba kwa
vizazi vingi sana sasa watu wamekuwa hawamtukuzi
Mungu moja kwa moja mbele ya jamii wakati wanapofika kwenye kilele cha
mafanikio yao hata kama
wanajua kwamba Mungu ndiye aliyewafikisha hapo. Mara zote utawasikia hata
Wakristo wakisema tu wanamshukuru Mungu kwa kufikia lengo ama kitu flani katika
maisha yao
lakini bila kwenda mbali na kueleza jinsi Mungu alivyohusika. Sivyo alivofanya Yusufu, yeye aliwaambia
waziwazi ndugu zake ya kwamba bila kujari alipitia hali gani, Mungu ndiye
aliyempeleka mpaka pale alipo kwa ajiri ya watu wake. Mwanzo 45: 5-8. Mungu
hakuwa amempleka Yusufu alipofika kwa njia rahisi ama ya mkato bali kwa njia ya
kujaribiwa na hata kuonewa na ndugu zake wa damu.
Ni rahisi kufikiri Yusufu
alikuwa akijaribiwa na shetani lakini yeye mwenyewe anasema sivyo bali alikuwa
akijaribiwa na Mungu. Pia mtunga zaburi anasema alikuwa akijaribiwa na ahadi ya
Bwana. Zab 109: 17-19. “ …..hata ulipofika wakati wa Bwana, ahadi ya Bwana
ilimjaribu” Kwa maneno mengine mtunga zaburi anatwambia Yusufu alikuwa
akijaribiwa na ahadi ya Bwana.
No comments:
Post a Comment