Biblia inaeleza wazi kwamba kuna “…wakati kwa kila kusudi
chini ya mbingu” Muhubiri 3:1. Ukilisoma andiko hili na kutazama hali ya maisha
ya kila siku ya Ukristo, utagundua kwamba kuna wakati maalumu wa kujaribiwa. Luka
22:52-53, Bwana Yesu anawaambia wale waliokuja kumkamata kwa nini hawakuwa na
wazo la kufanya hivyo hapo kabla, na anasema ni kwa sababu wakati wao ulikuwa
bado. Ukipata nafasi ya kujifunza somo liitwalo “Majira na nyakati za mkristo”
utaelewa zaidi kuhusu majira na wakati katika maeneo tofauti ya maisha ya
mkristo wakati anaposafiri kwenda mbinguni lakini kwenye somo hili tunaangazia
mambo kadhaa kama ifuatavyo:
(1)
Jaribu ni
nini?
Watu wengi wamekuwa na tafsiri tofauti kuhusu jaribu, lakini
si zote zilizo sahihi kwa mujibu wa maandiko. Wengi wa watu wa Mungu huita kila
tatizo au changamoto wanayokutana nayo kwenye maisha kuwa ni jaribu. Tafsri hii
si sahihi kwa mujibu wa maandiko. Ebu tazama jinsi ambavyo Biblia
inayatofautisha matatizo mengine ya kimaisha na majaribu ya kiimani.
Jaribu ni kipimo cha Imani.
Ebu tuseme jaribu ni mtihani wa imani, maandiko hutuonyesha kwamba Imani huja
kwa (hutokana na) kusikia (au kujifunza) neno la Kristo (Warumi 10:17) na hivyo
baada ya kuwa umeingia kwenye darasa la imani na kujifunza mambo kadhaa wa
kadhaa, huitajika ufanye mtihani ambao siyo tu hupima kiwango cha uelewa wako,
lakini huamua ikiwa uko tayari kwa kiwango kingine au bado, maana tunatoka
imani hata imani hata tukifikie kimo chake Kristo. Warumi 1:17. Hivyo mengi ya
yale tuyaitayo matatizo kwenye maisha yetu kama
wafuasi, ni mchakato wa kusogea hatua nyingine zaidi.
Mwanzo 22:1 “Baada ya mambo hayo , Mungu
alimjaribu Abrahamu….” Tazama msitari huu unavyoanza kwa kusema ‘baada ya mambo
hayo’, ndiyo kusema palikuwa na mambo kadhaa yaliyokuwa yametokea kabla ya
Abrahamu kujaribiwa. Ni ngumu kueleweka kwa akili za kibinadamu kwamba baada ya
Mungu kuwa amemwita Abrahamu kwenye sura ya 12 ya kitabu cha Mwanzo na Abrahamu
akatii, baada ya Mungu kumpa Abrahamu ahadi ya uzao mwingi kwenye sura ya
13, baada ya Mungu kumpigania Abrahamu
kwenye sura ya 14 na Abrahamu kumtolea Mungu fungu la kumi kupitia kwa
Melkizedeki, baada ya Mungu kumhakikishia Abrahamu kwamba uzao wake mwenyewe
ndiyo utakaomrithi na hapa naomba niseme
wazi kwamba Mungu kumhakikishia Ibrahimu juu ya kurithiwa na uzao wake mwenyewe
alikuwa amejibu moja ya vitendawili vikubwa vilivyokuwa vikimkabili Ibrahimu,
unaweza kumuona Ibrahim akijaribu ‘kumshawishi’ Mungu akubaliane na Ishmael
kuwa mwana wa ahadi kwenye Mwanzo 17:17. Ni kama Ibrahimu anamwambia Mungu “
Unajua hili suala linanishinda hata kulielewa, kwa nini tusimalize tu hili
jambo kwa kumtwaa Ishmael awe mwana wa ahadi?”. Jibu la Mungu kwa Ibrahim
lilikuwa kumpa Ibrahim jina la mtoto na
“…kwa habari ya Ishmael nimekusikia…..”. Ni kama Mungu akisema, Sawa Ibrahim
rafiki yangu, ninaelewa kwamba linakusumbua na kwamba unampenda pia mwanao
Ishamel, “…nimembariki…..”.
Ndiyo maana Roho
Mtakatifu anatuwekea jambo hili kwenye maandiko anaposema “Baada ya mambo hayo,
Mungu alimjaribu Ibrahim……” Ibrahim alikuwa ametembea na Mungu ya kutosha
kujifunza kwamba Mungu anajari mpaka yale mambo madogo madogo yatuumizayo kwa
ndani sana.
Yale ambayo hatuna hata maneno ama ujasiri wa kutosha kuyasema mbele za Mungu.
Mambo ambayo hatuna hakika kama Mungu mkuu
namna hii angependa kusikia hoja hizi kutoka kwetu. Pana nyakati katika maisha
ambapo tunajaribu kuwaza kwamba Mungu hajari chochote kuhusu hisia zetu
isipokuwa mapenzi yake tu yatimizwe,
basi!. Ibrahim alikuwa amejifunza kwamba Mungu alikuwa si dikteta anayetoa tu
amri na mipango yake kwenye maisha yetu, bali Mungu anayejari na ambaye
anafanya mambo kutubariki. Ibrahim alikuwa amepata daraja flani la Imani na
Baraka na sasa ilikuwa wakati wa Ibrahim kusonga mbele tena.
Sura ya 22, tunamuona Mungu akimjaribu
Abrahamu. Hapa tunaona mambo mawili makubwa.
Moja ni kwamba tangu Abrahamu kuitwa asijue aendako (Waebr 11:8) hadi kupigana vita
vya kumkomboa ndugu yake (Mwanz 14:13-16) na hata suala la Abrahamu kukosa
mtoto kwa miaka mingi, hayo hayakuwa majaribu, na kama
yalikuwa majaribu basi hakujaribiwa na Mungu. Maana Biblia inayaweka kwenye
fungu moja ambalo Biblia inaliita “Baada ya mambo hayo…” na ndipo inasema
Abrahamu alijaribiwa. Pili ni kwamba katika mambo yote hayo ambayo Abrahamu
alikutana nayo, Imani yake haikuwekwa njia panda, haikujaribiwa na ndiposa kila
anapovuka hatua flani utamuona Mungu ama akilithibitisha tu agano lake kwa
Abrahamu au akitoa maelekezo flani, lakini anapovuka kwenye jaribu unaona Mungu
akisema jambo tofauti (Mwanzo 22:12) anasema “…sasa najua kwamba unamcha
Bwana…”. Maana yake maelekezo ya Mungu mara hii yaliilenga imani ya Abrahamu na
siyo kitu kingine.
Ebu fikiri kwenye maisha yako binafsi, wakati ambapo mawazo
yako yanakuambia sasa uko sawa mbele za
Mungu na moyo wako ukitegemea kuona Baraka za Mungu, ndipo wakati huo
unapojaribiwa. Tunasoma kitu
kinachofanana na hiki kwenye habari za Yusufu, Mwanzo: 39:1-6b. Kwenye maandiko
haya utamuona Yusufu akibarikiwa na kupata kibali japokuwa alikuwa ameuzwa. Aliachiwa kila kitu na bwana wake
hata bwana wake “hakujua habari ya kitu chochote chake, ila hicho chakula
alichokula” na mstari wa saba unaanza kwa neno hili “Baada ya mambo hayo….”
Maana yake baada ya Mungu kuwa amemuonekania Yusufu namna hii, ulikuwa umefika
sasa wakati wa Yusufu kujaribiwa. Utagundua jinsi ambavyo Yusufu alipitia mambo
mbalimbali na si mambo yote hayo yalikuwa majaribu. Utaona jinsi ambavyo Yusufu
hakuwa na hofu ya “kumkosa Mungu” katika mambo yote aliyopitia isipokuwa suala la mke wa Potifa lilitishia
mahusiano yake na Mungu, lilimuweka njia panda ikiwa aamue kutembea na mke wa bosi wake
(angepata unafuu flani katika maisha kwa kipindi flani) au amuheshimu Mungu halafu
aingie kwenye ugomvi na huyu mama kwa vile kwa vyovyote mke wa Bosi wake
angejutia kitendo cha kuzifunua hisia zake kwa mtumishi wake na hivyo
angekasirika na Yusufu yamkini alifahamu hivyo.
Tofauti kati ya
Jaribu, Kwazo na Teso.
Labda si rahisi sana
kuelezea jaribu vizuri kwa kulitofautisha na magumu mengine tuyapatayo katika
maisha hata hivyo hapa chini tutajaribu kutofautisha kati ya Jaribu, Kwazo na
Teso kwa sifa za mambo haya matatu.
Jaribu huilenga imani
yako yaani mahusiano yako na Mungu moja kwa moja (Ayubu 1:9) kwa kuleta mambo
katika maisha yako ambayo ama yatakufanya umtilie shaka Mungu na ahadi zake,
utayari au hata uwezo wa Mungu kuzitekeleza, uhalali wa amri za Mungu kwenye
maisha yako na kadhalika. Ona jinsi ambavyo shetani hapa hana shida na mali za
Ayubu, bali ni kama anamwambia Mungu, “Nahisi Ayubu anakuheshimu kwa ajiri
ya baraka ulizompa na nina uhakika
ukimyang’anya basi atahamia kwenye kambi pinzani na wewe”. Ndiyo maana anasema
“…naye atakukufuru mbele ya uso wako” Ona ambavyo Mungu hana mashaka na imani
ya Ayubu lakini anamruhusu shetani kwenda na kumjaribu kwenye mali zake zote. Twaweza kujifunza
mengi kwenye majaribu ya Ayubu kama
tutakavyoona huko mbeleni.
Kwazo huilenga akili yako
kwa kutokeza mambo ambayo ama hayakubaliani na falsafa ama misimamo yako
mingineyo katika maisha. Ndiposa Yesu Kristo anawaambia wanafunzi wake kwamba
“…makwazo hayana budi kuja…” Luka 17:1-3. anawaambia makwazo ni matokeo ya
makosa ya kutokufahamu jinsi ya kuyaweka pamoja mazuri na madhaifu yetu katika
maisha na hivyo mara nyingi twakoseana na kughafirishana. Na hivyo mwokozi
anatushauri “…jilindeni, kama ndugu yako akikosa, muonye, akitubu msamehe”. Shida
kubwa zilizoko leo, zisingekuwako kama tungejifunza juu ya kuzungumza na
waamini wenzetu kanisani, wafanyakazi wenzetu mahala pa kazi na hata
wenzi wetu kwenye ndoa na familia juu ya mambo ambayo tunadhani hayakuwa sawa
walipoyasema ama kuyatenda, tujaribu kuwasikiliza wanapotupa sababu za wao
kutenda au kusema hivyo na kwa upendo tuwaonyeshe makosa yao. Hapo bila shaka
watatubu na sisi tutawasamehe na makwazo yatakomea hapo. Ni vivyo tunapowakosa
wenzetu na wakatueleza makosa yetu, tunatubu na kuwaomba watusamehe na makwazo
yanakomea hapo. Ebu tazama Lutu na Abrahamu walivyokwazana na wakamaliza tatizo
lao kwa mazungumzo. Mwanzo 12:1-12.
1Sam 30: 1-6 .Habari za Daudi kwenye sura hii zaweza
kutufunza vizuri juu ya hili, Daudi na kikosi cha askari wake 600 walikuwa
wamekimbilia Gathi ili wakae mbali na Sauli. Inaonekana mfalme wa Gathi alikuwa
akimuunga mkono Daudi na hivyo alikuwa amempa mji mmojawapo ili yeye na watu
wake waweze kuishi.
Siku moja vita vikalipuka kati ya mfalme wa Gathi na Israel
na Daudi akitaka kurudisha fadhila kwa mwenyeji wake akaamua kwenda na jeshi
lake kwa ajiri ya kupigana dhidi ya Israel, lakini kwa sababu za kiusalama,
washauri wa masuala ya usalama wa serikali ya Gathi hawakutaka Daudi aende nao
vitani na hivyo akaruhusiwa kurudi yeye na jeshi lake kwenye mji wao.
Walipofika, siyo tu mji haukuwepo bali hata familia ya Daudi na familia za
askari wake hazikuwapo, maadui walikuwa wameuvamia mji wakauchoma moto na
kuwachukua mateka watu wote na pia kuzichukua mali zote kuwa nyara. Biblia
haisemi ni kwa nini hawakuwaua watu wote kama
ilivyokuwa desturi ya vita, labda kwa sababu walikuwa hawakukutana na upinzani
wowote kwa vile askari hawakumo kwenye mji au lah! Lakini ni vyema kusema,
Mungu alikuwa amewaponya watu hawa na kuwalinda wasiuawe na adui. Askari wa
Daudi kwa mara ya kwanza wakatishia kuasi, walitaka kumpiga mawe kiongozi wao
ambaye wamempenda na kumfuata miaka yote. Wengi wa askari hao walikuwa kwa
hiyari yao wenyewe wamemfuata Daudi huko msituni na kujiunga naye wakiwa wameacha
nyuma maisha yao ya kawaida kwa hiyari yao, lakini hili lilikuwa
nimewakasirisha sana na japo halikuwa kosa la Daudi kwa kile ambacho kinaelezwa
kwamba “…kwa kuwa nafsi za hao watu zilighafilika sana….”(KJV). kwa tafsiri
nyingine watu hawa walikuwa wamekasirika ama kukwaza, lakini siyo kujaribiwa.
Twaweza pia kusema,
kwazo linalenga furaha na amani ya moyo. Zab 119:165. Tafsiri ya neno
“kuwakwaza” kwenye kiingereza (KJV) inasema “to offend them” inatumia neno
‘offend’ ambalo tafsiri yake ni ‘kosea’
ama ‘umiza kihisia’ ‘finya’ na ambalo linatokana na neno “offense” yaani kosa.
Kwa hiyo makwazo Ni mwitikio wetu Kwa makosa ama yetu wenyewe, au ya
wenzetu na matokeo yake kwenye maisha yetu ya kila siku.
Teso ni hali ambayo huruhusiwa kwa upendo na Mungu
kwenye maisha yetu kwa ajiri ya kukomesha mambo fulani yasiyopendeza katika
maisha yetu. Hii ni ajabu kwamba katika upendo wake, muumbaji wa vitu vyote
humtumia mwanadamu teso fulani katika maisha yake ili asiingie katika njia
isiyompasa. Zab 119:71, Ayubu 36: 15, Zab 118 :18 . Pia
Mungu huyatumia mateso kututendea kama
wana wa Mungu na ni kwa faida yetu wenyewe Ebr 12:10. Pia Mungu hutumia teso kama njia ya kuwafundisha watu (hata wale ambao sio
wanaoteswa) juu ya jambo flani la Kimungu Daniel 4-5
Kwa hiyo tumeona mambo kadhaa yanayotofautisha jaribu na
changamoto nyingine tuzipatazo katika maisha.
(i)
Kwanza jaribu lina
muda wake
(ii)
Pili jaribu linalenga imani yako katika Mungu moja kwa
moja
(iii)
Tatu jaribu huja baada ya kuwa Mungu amejifunua kwa jinsi flani kwako.
Tutazungumza suala la
Muda wa jaribu huko mbeleni kwa upana zaidi.
* Kwa hiyo twaweza kusema, Shida
(changamoto) yoyote haiwi jaribu hadi imekuweka njia panda, uchague kati ya
kumtii Mungu au kuchukua maamuzi mbadala yatakayokuepusha na shida
inayokukabili. Mwanzo 39:9b, Daniel 3:14-18, Ayubu 2:9-10, 1Pet 1:7