Wednesday, October 23, 2013

UNAWAZA NINI JUU YA BWANA!?.



Katika ulimwengu wa sasa tunaoishi, si rahisi kuwa Mkristo. Si kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa tu kwamba vita kati ya falme mbili yaani ufalme wa giza na Ufalme wa Nuru imefikia mahala pa juu kabisa katika historia ya kizazi chetu walau kwa miaka 100 iliyopita.

Tumesoma mara kadhaa juu ya mashujaa wa imani na gharama walizolipa kuufanya Ukristo uendelee kutajwa duniani, lakini kwa miongo kadhaa, imani hii haijakabiliwa na mashambulizi makubwa kama ilivyo sasa.

Imani inashambuliwa ndani na nje. Ndani ya Imani yenyewe, matendo na maneno yetu yaliyo matunda ya mawazo yetu yamekuwa ama kinyume na ukristo wenyewe ama yamekuwa duni kiasi hatusogei mbele kama tulivyopaswa. Mwandishi mmoja katika Biblia anawauliza watu wa kizazi chake kusema “Mnawaza nini juu ya BWANA…..!” na mimi naomba kukiuliza kizazi hiki cha waamini, MNAWAZA NINI JUU YA BWANA?. Hivyo ni lengo la waraka huu kuwaita waamini wote kujihoji swali hili muhimu. Kila mmoja wetu ajiulize “Ninawaza nini juu ya BWANA…?’. 

Mtume Paulo anatuandikia katika Warumi 12:2 kusema “….lakini mgeuzwe kwa kufanywa upya NIA zenu….”, sasa ukisoma neno NIA kwenye Kiswahili waweza kudhani ni kugeuka kwa malengo ama makusudio ya moyo na tafsiri hiyo ni sahihi, lakini andiko hili linasomeka hivi kwenye kiingereza (KJV)
 “…but be ye transformed by the renewing of your mind, that ye may prove what is that good, and acceptable, and perfect, will of God”. Ni kama Paulo mtume anasema “….mfanywe upya akili zenu….” na mkiisha fanywa upya akili zenu, mtatambua yaliyo mema, mazuri na yenye kumpendeza Mungu.

Kwa nini hatushauriwi kugeuzwa roho zetu, mavazi yetu, madhehebu yetu, shule tunazosoma, vyakula tunavyokula, nyumba tunazoishi na kadhalika, lakini tunashauriwa ‘kugeuzwa akili zetu’?.  Tunaandikiwa mahala pengine kusema “Itumieni akili sawasawa na wala msitende dhambi…”.
Ndugu zangu, kama kuna mali ya thamani ambayo Mungu ameiwekeza ndani yako ni akili yako. Wako watu ambao hupima mafanikio na uwezo wa mtu kwa kuangalia kiasi cha mali alizonazo, na wengi wa hao uhusisha umiliki wa mali na uwezo wa kiakili na hili ni kweli. Akili ndiyo nyenzo ambayo Mungu ameiweka ndani ya mtu kumsaidia kuchanganua mambo na uwezo wa mtu kuchanganua mambo huakisi uwezo wa mtu huyo kuhusiana na jamii na mazingira yake na hata kushindana na changamoto zake. 

Sasa usikwazwe ikiwa utadhani kwamba najaribu kupunguza nafasi ya utendaji wa Roho Mtakatifu katika maisha yako ya kila siku, lakini najaribu kukueleza juu ya ukweli kwamba Roho Mtakatifu anayo nafasi yake katika maisha ya Mkristo, lakini pia akili ya mtu inayo nafasi na mchango wake katika maisha ya Mkristo pia na viwili hili vyapaswa kwenda pamoja. 

Sikubaliani na wazo kwamba ukiamka asubuhi unahitaji kumuuliza Roho Mtakatifu aina ya nguo unayohitaji kuvaa kwa siku hiyo, bali unahitaji kutambua mpangilio wa shughuli zako kwa siku hiyo na kuvaa kulingana na hitajio la wakati. Ingekuwa ajabu ikiwa fundi makenika angeingia kazini kwake akivalia suti nadhifu si kwasababu hawezi kufanya kazi akivalia hivyo, bali mahitaji ya kazi yake ni vazi tofauti na hilo. Kadhalika, mwanasiasa ama mfanyabishara anayekwenda kwenye kikao cha kibishara cha kimataifa akiwa amevaa kaptula, siyo kwamba haweza kuendesha kikao kwa ajiri ya vazi lake, lakini mahala na wakati na hata tukio uhusika katika kuamua aina ya mavazi na hilo ni zao la akili. Ni jukumu la akili yako kutambua aina ya tukio, mahala linapofanyika, mazingira ya tukio lenyewe na kadhalika na kuvaa kulingana na hayo unayoyafahamu. 

Kanisa hata hivyo limeacha ama kwa makusudi au bahati mbaya kuwafundisha watu wake juu ya matumizi sahihi ya kipawa hiki chema na hivyo wengi wa wakristo wanamchukulia Mungu kama mwenye kuketi kando na kusubiri waje kwenye majumba ya ibada na kuabudu na hivyo wanaishi maisha yao yote wakipuyanga tu na kisha kukutana na Mungu wao Jumapili, ama wanamtaka Mungu afanye kila kitu kwenye maisha yao na kwa vile hilo haliwezi kutokea, basi wanadhani ama wana kasoro ama dhambi fulani inayomfanya Mungu asijifunue kwao ama yeye ni Mungu asiyejari kabisa maisha yao ya kila siku, lakini tatizo ni jinsi watu hawa wanavyowaza juu ya Bwana. 

Tunafahamu sote kwamba Yesu alikufa ili tuwe huru kutoka utumwa wa dhambi, lakini mara nyingi tunasahau kwamba Bwana wetu Yesu Kristo alipoanza kufundisha na hata alipowafundisha wanafunzi wake kuomba hakuwafundisha kuomba waende kwenye ufalme wa Mungu bali aliwaambia waombe kusema “Ufalme wako uje (hapa duniani), utakacho kifanyike hapa duniani kama huko mbinguni….”.
Kwa hiyo wakati tunapotafakari pamoja juu ya somo hili UNAWAZA NINI JUU YA BWANA? Lengo ni kukuonyesha mambo machache ambayo yamefunuliwa kwangu katika kuwaza kwangu juu ya BWANA.